Fasihi Simulizi Kiswahili

info

Fasihi Simulizi ni nini?

Fasihi ni sanaa inayotumia lugha kuwasilisha ujumbe unaomhusu binadamu.
Sanaa ni ufundi wa kuwasilisha fikra na hisia za binadamu kama vile maneno, maandishi, uchoraji, uchongaji, ufinyanzi n.k.

Fasihi simulizi ni sanaa kwa vile:

  1. Huwasilisha ujumbe kuhusu binadamu kuhusu utamaduni na uchumi
  2. Huwa na umbo mahsusi k.m. hadithi huwa na mwanzo, kati na mwisho na mashairi huwa na beti, mishororo, n.k.
  3. Hutumia lugha kwa ufundi k.v. ya kitamathali
  4. Husawiri mandhari/mazingira mahsusi kwa ufundi mkubwa
  5. Hujenga wahusika kwa ustadi mkuu ili kusawiri tabia za watu katika jamii

Tofauti Kati ya Fasihi na Sanaa Nyingine

FasihiSanaa Nyingine
Kutumia lughaKutotumia lugha
Sanaa tendiSi tendi
Kutumia wahusika kuwasilisha maudhuiHutumia maumbo kumithilisha watu
Kutumia maudhui na fani kuwasilisha ujumbeKutumia maumbo na sura za vitu
Kujikita katika mazingira na wakati maalumHazijikiti katika muktadha na wakati maalum

Makundi Ya Fasihi

  1. Fasihi simulizi – Fasihi inayowasiolishwa kwa njia ya mdomo.
  2. Fasihi andishi – Fasihi inayowasilishwa kwa njia ya maandishi.

Tofauti Kati Ya Fasihi Simulizi Na Fasihi Andishi

  1. Fasihi simulizi huwasilishwa kwa njia ya mdomo ilhali fasihi andishi huwasilishwa kwa njia ya maandishi
  2. Fasihi simulizi huhifadhiwa akilini ilhali fasihi aandishi huhifadhiwa kwa maandishi
  3. Fasihi simulizi ni mali ya jamii ilhali fasihi andishi ni mali ya mtu binafsi/mwandishi
  4. Fasihi simulizi ina wahusika wa kila aina k.v binadamu, wanyama na ndege, mazimwi na majitu, miungu, mizimu, mashetani na vitu visivyo na uhai k.v. mawe na miti ilhali fasihi andishi ina wahusika binadamu kwa kiasi kikubwa
  5. Fasihi simulizi ina tanzu nyingi kuliko fasihi andishi
  6. Uwasilishaji wa fasihi simulizi huweza kuandamana na utendaji k.v matumizi ya ishara, nyimbo, makofi, kuimba, kubeba zana katika majigambo n.k ilhali ule wa fasihi andishi hauandamani na utendaji isipokuwa inapowasilishwa mbele ya hadhira
  7. Fasihi simulizi huwasilishwa mbele ya hadhira ilhali fasihi andishi si lazima iwasilishwe mbele ya hadhira
  8. Fasihi simulizi huwasilishwa mahali maalum k.v jandoni, matangani, arusini, n.k ilhali fasihi andishi haina mahali maalum
  9. Fasihi simulizi huandamana na shughuli fulani ya kitamaduni ilhali fasihi andishi haiandamani na shughuli ya kitamaduni
  10. Fasihi andishi huhitaji muda kutunga ilhali baadhi ya fasihi simulizi huzuka papo hapo k.m. semi, maigambo
  11. Fasihi simulizi ina uwezo mkubwa wa kubadilishwa na fanani anapowasilisha ufaraguzi) bali fasihi andishi haibadiliki isipokuwa mwandishi aiandike upya
  12. Fasihi simulizi ina historia ndefu kuliko fasihi andishi kwa kuwepo tangu mwanzo wa maisha ya binadamu
  13. Fasihi simulizi huwasilishwa wakati maalum k.v. usiku, kipindi fulani cha mwaka ilhali andishi haina wakati maalum

Jinsi Fasihi Simulizi na Andishi Zinavyofanana

  1. Zote mbili hushughulikia masuala yanayohusu maisha maisha ya binadamu
  2. Zote mbili Huhumia lugha kwa ubunifu kuwasilisha maudhui
  3. Zote mbili huwa na vipengele viwili vikuu, maudhui na fani (jumla ya mbinu msanii alizotumia kuwasilisha maudhui)
  4. Zote mbili majukumu sawa k.v. kuburudisha, kuadilisha, kuhifadhi na kuendeleza utamaduni, n.k
  5. Zote mbili zina utendaji-pale tamthilia na riwaya zinapoigizwa
  6. Zote mbili huzaliwa, hukua na hufa kutegemea mabadiliko ya wakati
  7. Zote mbili huwa na wawasilishaji-fanani k.m. mtambaji/mganaji au manju/yeli katika fasihi simulizi na mwandishi upande wa fasihi andishi
  8. Fasihi simulizi imekopa tanzu za fasihi simulizi k.v. methali, mashairi, n.k

Majukumu ya Fasihi Simulizi

  1. Kuburudisha-kustarehesha, kufurahisha, kuchangamsha, kutuliza, kusisimua na kupumbaza akili na kiwiliwili – nyimbo, hadithi, vitendawili
  2. Kufunza maadili kwa wanajamii kwa kuwahimiza kuiga sifa chanya na kukataa sifa hasi za wahusika
  3. Kukuza uwezo wa kufikiri/kudadisi k.m vitendawili na chemshabongo
  4. Kufariji k.m mbolezi na methali k.m. ‘Baada ya dhiki faraja’
  5. Vipengele vya fasihi simulizi k.v mashairi, nyimbo, nahau, hutumiwa katika uandishi wa fasihi andishi
  6. Kuhifadhi historia ya jamii k.m. mighani, visaviini, mapisi, tarihi n.k.
  7. Kukejeli tabia zinazokiuka matarajio ya jamii k.v soga, methali, n.k.
  8. Kuendeleza tamaduni za jamii kwani husawiri imani na desturi za jamii. k.v kitendawili ‘Nyumbani mwetu mna papai lililoiva lakini siwezi kulichuma.’ – Mtu hawezi kumwoa dadake
  9. Kuunganisha watu pamoja kwa kuwajumuisha pamoja wakati wa ngoma, kuimba, utambaji, n.k.
  10. Kukuza lugha k.v. misimu inapokita kimatumizi na kujumuishwa katika lugha sanifu
  11. Kukuza uwezo wa kutumia lugha kadiri mtu anapoendelea kuwasilisha k.v. hotuba, vitanza ndimi husaidia kuboresha matamshi na kutofautisha maana za maneno
  12. Kuza uwezo wa kubuni k.v. malumano ya utani, vitanza, ndimi ngonjera, n.k.
  13. Kukuza uzalendo kwa kufanya wanajamii kuonea fahari jamii zao na kuiga mashujaa au watu waliotendea jamii makuu
  14. Kuonya na kutahadharisha wanajamii dhidi ya tabia hasi k.v. ulafi, uchoyo, n.k.

Sababu za Ufaraguzi / Kubadilika kwa Fasihi Simulizi

Kuwasilishwa vibaya

Fanani kusahau na kubadilisha yaliyomo na mtiririko

Kubadilisha ili kukidhi mahitaji ya hadhira k.m. umri na uelewa wao- kutumia lugha nyepesi kwa watoto na pevu kwa watu wazima

Mabadiliko ya mandhari/mazingira-vitu vilivyo katika mazingira halisi kukosekana katika mazingira ya usimulizi na msimulizi kutumia vitu katika mazingira yake vinavyokaribiana navyo

Kutoeleweka na hivyo kuhifadhiwa vibaya

Mabadiliko ya wakati k.m kitendawili cha wakati wa mkoloni kutumia mzungu na cha wakati wa mwarabu kutumia mwarabu na maana ni ile ile-Mzungu/mwarabu amesimama kwa mguu mmoja-mwavuli

Mabadiliko ya falsafa ya vizazi na maingiliano katika jamii kusababisha kurithisha tu yale ambayo ni muhimu na kuacha mengine

Kila fanani huwa na mtindo wake wa kuwasilisha/kisanii

Ubunifu wa fanani ili uwasilishaji uweze kuvutia saidi na uwezo wake wa lugha

Teknolojia kusababisha kuhifadhiwa na hivyo kuiua

Wahusika katika Fasihi Simulizi

Wahusika ni viumbe wa sanaa ambao hutumiwa katika kazi ya fasihi kuwasilisha maswala mbalimbali.

  • Fanani – anayetunga na kuwasilisha fasihi simulizi
  • Hadhira – kusikiliza, kutazama, kushiriki wa kuimba, kuuliza maswali, kutegua vitendawili, kupiga makofi, n.k. kuna aina mbili za hadhira:
    1. Hadhira tendi/hai
    2. Hadhira tuli
  • Wanyama – wanaofanya kama binadamu na kuwakilisha sifa kama vile ujanja, ulaghai, tamaa na ujinga na wanaobakia wanyama tu
  • Binadamu
  • Mazimwi na majitu – viumbe vyenye matendo na maumbile ya kutisha kama vile jicho moja, vichwa viwili au zaidi, nusu mtu na nusu myama, wenye tamaa iliyokithiri ya kuweza kumeza kila kitu, kuhifadhi na kutunza binadamu ananyoyapendeza
  • Wahusika vitu (visivyo na uhai) k.m. mawe, miti, vijaluba, vibuyu-hutumiwa kuibua imani za kidini
  • Mizimu – roho za waliokufa – hutembea, hula na huathiri binadamu
  • Miungu – viumbe vyenye uwezo mkubwa dhidi ya binadamu k.m. katika mighani na visasili

Njia za Kukusanya Fasihi Simulizi

a)Kuchunza / Utazamaji

– Kutazama kwa makini yanayotokea na kuandika.

Umuhimu

  • Kupata habari za kutegemewa na kuaminika
  • Ni rahisi kurekodi k.v. kwa vinasa sauti, video, n.k.
  • Ni njia bora kwa wasiojua kusoma na kuandika
  • Kuweza kupata sifa za uwasilishaji k.v. toni/kiimbo, ishara n.k.
  • Kuweza kupata hisia halisi za uwasilishaji

Udhaifu

  • Shida ya mawasiliano
  • Ugeni wa mtafiti kusababisha washiriki kumshuku na kusitisha uwasilishaji
  • Ghali kwa kumbidi mtafiti kusafiri
  • huhitaji muda mrefu

b) Kusikiliza Wasanii Wakiwasilisha Tungo Zao

Umuhimu

  • Kuweza kupata sifa za uwasilishaji k.v. toni/kiimbo, ishara n.k.
  • Kupata habari za kutegemewa na kuaminika
  • Ni rahisi kurekodi k.v. kwa vinasa sauti, video, n.k.
  • Kikwazo cha mawasiliano-Si njia bora kwa wasiojua kusoma na kuandika
  • Kuweza kupata hisia halisi za uwasilishaji

Udhaifu

  • Shida ya mawasiliano-Si njia bora kwa wasiojua kusoma na kuandika
  • Huhitaji muda mrefu-kusafiri na kusikiliza
  • Ugeni wa mtafiti kusababisha washiriki kutowasilisha ipasavyo
  • Ghali kwa gharama ya usafiri

c) Mahojiano

– Kuhoji wanaofahamu mengi kuhusu fasihi simulizi.

Umuhimu

  • Kuweza kung’amua wakati mhojiwa anatoa habari zisizo za kweli
  • Kuweza kufafanulia mhojiwa maswali ili kuweza kupata habari sahihi zaidi
  • Kuweza kupata sifa za uwasilishaji k.v. toni/kiimbo, ishara n.k.
  • Ni rahisi kurekodi k.v. kwa vinasa sauti, video, n.k.
  • Kupata habari za kutegewa na kuaminika

Udhaifu

  • Huhitaji muda mrefu
  • Mhojiwa kutotoa habari kwa kutomwamini mtafiti kwa ugeni wake
  • Kikwazo cha mawasiliano-si njia bora kwa wasiojua kusoma na kuandika
  • Ghali kwa gharama ya usafiri.

d) Kurekodi Katika Kanda za Sauti / Tepurekoda

Umuhimu

  • Kuweza kudumu na kufikia vizazi vingi
  • Sifa za uwasilishaji/uhai kama vile toni na kiimbo kuhifadhiwa
  • Mkusunyanyaji aweza kurudia uwasilishaji ikiwa hakuelewa
  • Kupata habari za kutegewa na kuaminika
  • Kuweza kupata hisia halisi za uwasilishaji

Udhaifu

  • Chaweza kukosa nguvu za umeme na utafiti kuathirika
  • Hakiwezi kunasa uigizaji
  • Fanani huenda asiwasilishe vyema akijua anarekodiwa
  • Ghali kwa kuhitaji kununua kifaa na kumbidi mtafiti kusafiri

e) Kurekodi kwa Filamu na Video

– Hunasa picha zenye miondoko na sauti.

Umuhimu

  • Video huhifadhi uigizaji, ishara na kiimbo/toni
  • Kuonyesha uhalisi wa mandhari
  • Mkusunyanyaji aweza kurudia uwasilishaji ikiwa hakuelewa
  • Kazi iliyokusanywa hivi hudumu kwa muda mrefu
  • Njia bora kwa wasiojua kusoma na kuandika
  • Kupata habari za kutegewa na kuaminika

Udhaifu

  • Chombo chaweza kukosa nguvu za umeme na utafiti kuathirika
  • Fanani huenda asiwasilishe vyema akijua anarekodiwa
  • Njia ghali
  • Fanani huenda asiwasilishe vyema akijua anarekodiwa
  • Ghali kwa gharama ya ya usafiri na kununua filamu na kamera ya video
  • Data yaweza kufisidiwa na hivyo kutowafikia walengwa

f) Kupiga Picha kwa Kamera

– Hunasa picha zisizo na miondoko na sauti.

Umuhimu

  • Huonyesha uhalisi wa mandhari
  • Huweza kuhifadhi ishara
  • Mkusunyanyaji aweza kurudia uwasilishaji ikiwa hakuelewa
  • Kupata habari za kuaminiwa na kutegemeka

Udhaifu

  • Ghali kwa gharama ya ya usafiri na kununua kamera
  • Sifa za uhai kama vile kiimbo haziwezi kuhifadhiwa
  • Yaweza kukosa nguvu za umeme na utafiti kuathirika
  • Data yaweza kufisidiwa na hivyo kutowafikia walengwa

g) Kushiriki Katika Kazi ya Fasihi Simulizi k.v. ngoma, soga, n.k

Umuhimu

  • Kuweza kupata hisia halisi za uwasilishaji
  • Kupata habari za kutegewa na kuaminika
  • Njia bora kwa wasiojua kusoma na kuandika
  • Kukuza utangamano wa mtafiti na wanajamii
  • Kuweza kunasa na kuhifadhi sifa za kiimbo, toni na ishara

Udhaifu

  • Kuchukua muda mrefu
  • Ugeni wa msanii kusababisha washiriki kuwa na wasiwasi na kutotenda kama kawaida
  • Njia ghali kwa kuhitaji mtafiti kusafiri mbali
  • Mtafiti aweza kusahau kwa kuhifadhi akilini

h) Kutumia Hojaji

Umuhimu

  • Gharama ya chini
  • Yaweza kutumika katika mahojiano
  • Huokoa muda kwani mtafiti aweza kuituma na kuachia mhojiwa kujaza

Udhaifu

  • Utata wa maswali kusababisha majibu yasiyo sahihi
  • Si nzuri kwa wasiojua kusoma na kuandika
  • Kutopata sifa za uwasilishaji kama vile kiimbo, toni na ishara
  • Wahojiwa kukataa kuijaza kutokana na mwelekeo hasi dhidhi ya hojaji na hivyo kukwamiza utafiti

Vifaa vya Kukusanya Fasihi Simulizi na Udhaifu Wake

  1. Vinasa sauti/tepu rekoda
  2. Kamera
  3. Filamu na video
  4. Diski za kompyuta
  5. Kalamu na karatasi

Umuhimu

  • Kuweza kudumu na kufikia vizazi vingi
  • Si rahisi kusahaulika-hubakia vile vile
  • Si njia ghali kama vile video

Udhaifu

  • Sifa za uwasilishaji kama vile toni, kiimbo/toni na ishara haziwezi kuhifadhika hivyo kupotea
  • Hupunguza hadhira kwa kulenga tu wanaojua kusoma na kuandika na hivyo kuathiri usambazaji wake

Mbinu za Kuhifadhi Fasihi Simulizi

a) Huhifadhiwa na binadamu akilini k.m. ngano hupokewa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
b) Katika maumbile au mazingira k.m. fisi daima huchechemea , kinyonga naye hutembea pole pole.

c) Katika vifaa meme k.m. nyimbo, hadithi, maigizo n.k. huweza kuhifadhiwa katika kanda za sauti, video, sidi na diski za kompyuta.
d) Katika michoro k.m. picha huhifadhi matukio maalum k.v. za kabila fulani likiwinda au likisherehekea.

Umuhimu wa Kukusanya / Kuhifadhi Fasihi Simulizi

  1. Ili isipotee k.m. kwa kusahaulika
  2. Kuirekodi ili kuiendeleza kwa kuirithisha kwa vizazi vijavyo
  3. Ili kulinganisha fasihi simulizi za jamii mbalimbali na kuonyesha tofauti zake
  4. Ili kuhakikisha mtiririko katika uwasilishaji
  5. Kutunza historia ya jamii ili vizazi vijavyo viijue
  6. Ili kuziba mapengo ya utafiti yaliyomo kwa vile kuna tungo ambazo hazijatafitiwa kwa kina
  7. Kuendeleza elimu ya jadi ya jamii
  8. Kuingiliana na jamii iliyo chanzo cha fasihi humwezesha kuelewa na utamaduni na fasihi yake kwa ujumla
  9. Humwezesha mwanafunzi kuona vipengele hai vya fasihi k.v. uigizaji, toni na kiimbo ambavyo husaidia kuielewa kwa kina
  10. Husaidia kuhifadhi tamaduni za jamii kwa nia ya kuzipitisha kwa vizazi vijavyo
  11. Husaidia kuelewa utamaduni wa jamii nyingine
  12. Humwezesha mwanafunzi kupata maarifa ya kufanya utafiti katika taaluma nyingine k.v. sosholojia
  13. Kujua fasihi simulizi za jamii nyingine humfanya mtafiti kuzielewa na kuzikubali jamii hizo na hivyo kuendeleza amani katika nchi
  14. Ili kusahihisha mawazo mapotovu kuhusu baadhi ya tanzu na vipera vya fasihi simulizi

Matatizo Yanayomkabili Mkusanyaji wa Fasihi Simulizi

  1. Gharama ya utafiti kuwa kubwa kiasi cha mtafiti kutoimudu k.v. kusafiria, kununulia vifaa
  2. Kutojaziwa hojaji kutokana na mtazamo hasi wa jamii dhidi ya ujazaji wake
  3. Wanajamii kukataa kutoa habari wakishuku mtafiti anawapeleleza au kwa kuona haya
  4. Wanajamii wengine kudai walipwe kabla ya kutoa habari na hivyo kukwamiza utafiti
  5. Mbinu nyingine k.v. hojaji huhitaji watu wanaojua kusoma na kuandika na ikiwa mhojiwa hajui utafiti utakwamizwa
  6. Uchache wa wazee na wataalamu wa fasihi simulizi kusababisha kukosekana au kupatikana kwa data isiyo ya kutegemewa
  7. Utawala kukataa kutoa idhini ya kufanya utafiti
  8. Kukosa ufadhili na utafiti kutofanywa kwa kutomudu gharama
  9. Muda wa utafiti kutotosha na hivyo kutopata habari za kutosha kuhusiana na mada yake
  10. Kikwazo cha mawasiliano ikiwa mtafiti na mhojiwa hawatumii lugha moja na mhojiwa hajui lugha nyingine na kumbidi mtafiti kukodi mkalimani na gharama kuongezeka
  11. Ukosefu wa vyombo vya usafiri kunakochelewesha utafiti na kutomalizika katika muda uliopangwa
  12. Ukosefu wa usalama k.v. kuvamiwa kwa kushukiwa anapeleleza na kuibiwa vifaa

Changamoto Zinazokabili Ukusanyaji wa Fasihi Simulizi

  1. Ukosefu wa utafiti wa kutosha kwani kuna vipera ambavyo bado havijaandikwa
  2. Uchache wa wataalamu wa kutafitia na kuendeleza utafiti
  3. Watu kuhamia mijini na kuingiliana na wa jamii nyingine na kufanya uhifadhi na urithishaji wa fasihi kutowezekana
  4. Mtaala wa elimu kupuuza lugha ya kiasili inayotumiwa kuhifadhia na kurithisha fasihi simulizi na hivyo kukatiza ukuaji wake
  5. Fasihi simulizi kuhusishwa na ukale na hivyo kutoona haja ya kuirithisha na kuihifadhi
  6. Kuhifadhiwa kwa fasihi simulizi akilini kusababisha kusahaulika, kubadilika hata kufa kwake

Jinsi Jamii ya Sasa Inavyojaribu Kuhifadhi Fasihi Simulizi

  1. Tamasha za muziziki kunakokaririwa na kuimbwa mashairi
  2. Sherehe za arusi, jando, mazishi mawaida
  3. Utegaji na uteguaji wa vitendawili kupitia redio na runinga
  4. Sarakasi za wasanii huhifadhi kipera cha vichekesho
  5. Ngoma za kienyeji kama isukuti katika hafla za kisiasa na harusi
  6. Utambaji wa hadithi hasa katika sehemu za mashambani

Tanzu za Fasihi Simulizi

– Tanzu ni aina za tungo zenye muundo uliokaribia kufanana.

  • Hadithi
  • Semi
  • Ushairi
  • Mazungumzo
  • Maigizo