Please Limited time Offer!

Maudhui Katika Mapambazuko- Mapenzi na Ndoa, Mabadiliko,Usaliti,Dini

Maudhui ya Mapenzi na Ndoa

Mapenzi ndiyo chemchemi inayochangia ndoa. Kuna ndoa ya babake Lilia ambayo ilitawaliwa na mapenzi, kwani wakati huu mkewe ashaaga. Kila mara mhubiri huyu anamkumbuka. Hata anashindwa kuoa mke mwingine kutokana na mapenzi yao ya dhati. Anapatwa na huzuni tele baada ya kuaga kutokana na ajali ya barabarani. Mwandishi anasema kuwa lau si ulimi wa bintiye usiotulia, dhiki ya kuachwa na mkewe ingemsukuma kaburini. Fahari kuu ya ndoa inadhihirika kupitia kujaliwa kwao binti huyu, Lilia, ambaye anfanana na mamake.

Ndoa kuu, hata hivyo, ni kati ya Luka na Lilia. Mapenzi yao yanaanza Lilia anapomwona Luka kwenye kanisa la babake, huku amevalia kimaskini. Sauti yake tamu inamvutia mara moja na hapo haachi kumwaza. Mapenzi yake kwa Luka yanamsukuma kumwomba babake amsaidie.

Babake anampeleka katika shule ya msingi na kumpa mamake kazi ya kusafisha kanisa.

Anamwelimisha hadi chuo kikuu, yote kwa ajili ya bintiye anayempenda Luka kwa dhati.

Usuhuba kati ya wawili hawa unaanza mapema, tangu wakiwa wachanga. Unamtia kiwewe babake Lilia, ambaye anajaribu kila mbinu kuwatenganisha bila mafanikio. Anapompeleka Luka upande mwingine wa nchi kwa mhubiri mwenzake, bado wanawasiliana kwa barua na simu. Bintiye anamsisitizia amri ya Mungu ya mapenzi na kumtaka awape baraka zake. Licha ya hisia za hofu kwa Luka, anawaruhusu kuoana.

Ndoa yao inaenda vizuri hadi babake Lilia anapofariki. Hapo Luka anabadilika na kuwa mwovu. Anamshinikiza mkewe kuacha kazi na kumtawisha. Hatimaye anaamua kujitosa katika siasa na mkewe anatakiwa kuwajibika, licha ya kuwa hapendi siasa. Anapokataa kushirikiana naye baada ya muda, anamkumbusha kuwa wanawake ni wengi na kumwacha pekee nyumbani. Analazimika kukimbizwa hospitalini na majirani na anapoteza uja uzito wake wa miezi minne, lakini Luka hahuzuniki sana.

Anaamini bado upo muda wa kupata watoto.

Mambo yao yanaharibika kabisa Luka anapokuwa gavana. Anaanza kuwa na vimada, huku akimlazimisha mkewe kuishi vijijini ili awe karibu na raia. Anamtembelea wikendi lakini hana muda naye, shughuli muhimu kwake ni kujiandaa kwa ajili ya wiki inayofuata. Mkewe anapomtembelea bila habari na kumpata na mwanamke mwingine, hajali chochote bali anamfokea mkewe na kumtaka arejee nyumbani na kuacha ujumbe Jioni hiyo anaporudi nyumbani, Luka anampiga mkewe vibaya, huku akimkanya dhidi ya kufika ofisini kwake bila taarifa na kutoheshimu wageni wake. Huu unaondokea kuwa mwanzo wa vipigo vya mara kwa mara. Ata kuhusiana na marafiki na majirani ananyimwa. Mumewe anaandamana na yule kimada wake katika hafla zote bila haya.

Lilia anaamua kuripoti polisi lakini anaghairi anapogundua mkuu wa polisi anajuana na mumewe. Anahofia usalama wake kutokana na kisa hicho, akijua mumewe atajua, pamoja na kukosa simu yake akiwa bafuni. Hofu yake inaondokea kuwa ukweli, kwani Luka anaporejea, anampiga vibaya hadi anapozirai na kumwacha. Anapopata fahamu, anamwita mama mkwe anayemwauni kwa kumpeleka hospitali. Hata haamini Luka anaweza kumfanyia Lilia hivi!

Haibainiki ndoa ya Luka inachukua mkondo gani mwishowe. Mkewe anatibiwa na kuruhusiwa kuondoka hospitalini, hali Luka mwenyewe amelazwa baada ya kupata ajali. Kimada wake naye amemtoroka baada ya kusikia huenda asiweze kutembea tena maishani.

Maudhui Katika Mapambazuko- Nafasi ya Mwanamke Katika Jamii.

Mwanamke katika jamii hii amepatiwa nafasi finyu sana, licha ya kuwa na mchango wa kipekee. Kwanza, mwanamke anadhihirika kuwa mpenzi wa dhati ya moyo. Mhubiri anamkumbuka mkewe waliyependana kwa dhati na ambaye anapofariki, anashindwa kabisa kuoa mke mwingine wa kujaza

pengo lake. Anashinikizwa na wahubiri wenzake, wazee wa kanisa na hata washirika wake lakini anashindwa kabisa kumwoa mwingine.

Lilia anapomwona Luka mara ya kwanza tu, anampenda kwa dhati hasa kutokana na sauti yake ya kupendeza. Anamshinikiza babake hadi anapompa mamake kazi ya kusafisha kanisa na hata kumpeleka Luka shule. Majaribio ya babake kuwatenganisha hayazai matunda kwani Lilia yuko mstari wa mbele kumpigania Luka wake hadi wanaporuhusiwa kuoana na baba kuwapa baraka zake.

Hata Luka anapoingilia siasa, Lilia anamsaidia licha ya kutopenda siasa. Anamvumilia na ukware wake na kubaki kuwa mwaminifu siku zote. Anampiga mara kwa mara, lakini anazidi kumshughulikia kama mumewe hadi anampiga na kumsababisha kulazwa hospitalini.

Wanakutana huko baada ya Luka kupata ajali ya barabarani na kupoteza uwezo wa kutembea. Hatujui ndoa yao inachukua mkondo gani.

Mamake Luka pia ana mapenzi ya kipekee. Anampenda mwanawe Luka na anajitolea kumlea vyema licha ya umaskini wake. Lilia anapopoteza fahamu baada ya kipigo, anachukua simu na kumpigia. Anafika mara moja na kumhudumia. Anampigia mwanawe na kumlazimisha kutuma ambulensi, kisha kumpeleka Lilia hospitalini na kumuuguza.

Mwanamke pia anachukuliwa kama kiumbe dhaifu cha kuendeshwa na kuelekezwa na mwanamume. Luka anampa mkewe maagizo anayotaka kila mara. Anamkataza kujumuika na marafiki na anapofanya hivyo anampiga vibaya. Anamlazimisha kukaa nyumbani kama mtawa na kumtaka kumpigia simu akitaka kufika ofisini. Anapokosa simu yake akioga, anaingiwa na hofu kuu, kwani anajua yatakayofuatia. Luka anampiga mara kwa mara hadi mwisho anapolazwa hospitalini.

Mwanamke pia anasawiriwa kama chombo cha kumstarehesha mwanamume. Luka anamwambia mkewe kuwa wanawake ni wengi anapokataa kuandamana naye katika kampeni. Kulingana naye, ni rahisi kwake kupata wanawake wengine. Anapokuwa gavana, ana vimada wengi wala hajali hili linavyomwathiri mkewe. Anapomtembelea anampata na mwanamke mwingine. Badala ya kuwa na haya anamfokea na kumlaumu. Mwanamke yule naye pia anaendelea kuhusiana na Luka kimapenzi licha ya kujua ana mke.

Mwanamke pia anachorwa kama msaliti. Kimada wa Luka anajua kuwa ana mke lakini bado anasuhubiana naye na hata kuandamana naye katika shughuli rasmi. Hajali machungu anayomletea mkewe Luka. Isitoshe, anamtoroka Luka anapomhitaji zaidi, pale anapopata ajali na kupoteza uwezo wa kutembea.

Maudhui Katika Mapambazuko-USALITI

Luka anamsaliti babake Lilia. Mzee huyu anajitolea kumfaa kwa kila hali tangu akiwa mchanga. Anamsomesha na kumpa uongozi wa mahubiri katika kanisa lake. Anapofariki, anauza kanisa lake kwa nia ya kujifaidi binafsi. Pia anamsaliti kwa kuvunja ahadi aliyotoa ya kumlinda bintiye, kwani baada ya kumwoa anaanza kumtesa.

Luka pia anamsaliti mkewe Lilia. Kwanza, anamsaliti kwa kumwendea kinyume licha ya uvumilivu wa madhila ya mumewe na pia uaminifu wake. Pia, mkewe anapigania penzi tangu wakiwa wachanga. Anamshinda hata babake anayemshuku Luka. Licha ya haya yote, Luka anamtesa kwa mapigo ya kila siku hadi mwishowe anapolazwa hospitalini kwa mapigo haya.

Luka pia anasaliti dini na imani kwa kutumia kanisa kwa ajili ya manufaa ya kibinafsi. Kanisa linakua na kuimarika chini ya mahubiri yake, lakini linapokua, analigeuza biashara. Hatimaye analiuza na kuingilia siasa. Anasaliti dini na Imani pia kwa kubadilika na kuwa laghai, mkware, dhalimu miongoni mwa maovu mengine.

Kimada wa Luka anamsaliti kwa kumwacha anapomhitaji zaidi. Licha ya kumtelekeza mkewe kwa sababu ya kimada huyu, anamwacha kwenye kitanda cha hospitali anapopoteza uwezo wake wa kutembea.

Isitoshe, anamsaliti Lilia kwa kuhusiana na mumewe akijua vyema amemwoa.

Maudhui ya Dini – Mwongozo wa Mapambazuko

Jamii hii imejikita katika dini ya kikristo. Dini inachukua mkondo wake wa kuwapa waja tumaini na kuwatia shime. Dini pia inasaidie walio katika taabu kuwa na tumaini la maisha.

Lilia anakutana na Luka mara ya kwanza katika kanisa. Wako katika darasa la mabaleghe anapofika. Sadfa kuwa ni pale alipokaa tu Lilia penye nafasi anaiona kama ni Mungu anamjaribu. Anaketi na masomo kuendelea. Mwishoni mwa somo anapatiwa nafasi ya kujitambulisha. Anamtukuza Mungu kwa wimbo unaowapendeza waliomo humu, hata mhubiri anayekuja kuwajulisha muda umekwisha.

Lilia pia amelelewa katika misingi ya kikristo, kwani babake, Lee Imani ni mhubiri. Anamlea pekee baada ya mkewe kuaga kutokana na ajali ya barabarani.

Dini ndiyo inayopalilia penzi kati ya Luka na Lilia. Lilia anamwomba babake wamsaidie Luka kama dini inavyoelekeza. Babake anakubali kumpeleka shule na pia kumpa mamake kazi ya kusafisha kanisa.

Wanapojuana wakiwa watoto, Luka na Lilia ni marafiki wa kufa kuzikana. Wanapoingia ujanani, babake Lilia anahofia usalama wa bintiye na kujaribu kuwatenganisha kwa kumpeleka Luka upande mwingine wa nchi kwa mhubiri rafikiye. Bado wanawasiliana kwa simu na barua.

Mhubiri huyu anapotilia shaka mwelekeo wa uhusiano wa bintiye na Luka, bintiye anamkumbusha mahubiri yake mwenyewe kila mara kuwa Mungu ni upendo. Anamwambia kuwa hafai kumbagua Luka au kuona kama hamfai. Lee Imani analazimika kumuuliza Luka kuhusu nia yake kwa Lilia, naye anasisitiza kuwa ana nia safi kabisa. Licha ya mashaka aliyo nayo, hana lingine ila kuwapa Baraka zake.

Lilia anamshawishi babake kumpa Luka jukumu la kuhubiri kanisani, jukumu ambalo anatekeleza vilivyo. Anahubiri na baada ya muda, kanisa linafurika hadi mahema kuongezewa. Washirika wanampenda sana. Watu wanatoka nchi za mbali kufuatilia miujiza huku.

Lee anapofariki, Luka anageuza kanisa kuwa kitega uchumi. Anamwachisha mkewe kazi yake ya umeneja wa benki ili aje kutunza pesa za kanisa, japo kuna mhasibu anayefanya kazi vizuri. Baada ya muda, anauza kanisa lile na kuingilia siasa. Anasahau kabisa mambo ya dini na kubadilika kabisa. Anawatenga watu waliomchagua, anamtesa mkewe na kuwa mkware kupindukia. Mkewe naye anaishi kumwombea kwa imani kuwa atabadilika siku moja.

Migogoro-Maudhui Katika Mapambazuko

Mwanzo wa hadithi unadhihirisha mgogoro mkuu katika kisa hiki. Lilia yuko katika hali ya wasiwasi mkuu huku akimsubiri mumewe. Amezoea vitimbi vya mumewe anayemjia kwa makeke kila siku. Anapopita karibu na kioo akielekea kwenye chumba cha kulala, mabadiliko katika uso wake yanadhihirisha

migogoro ya awali kati yake na mumewe. Kwanza, kioo chenyewe kimepasuka. Ana kovu shavuni na donda linaloelekea kupona shavuni, zote kumbukumbu za mapigo ya awali.

Lilia anapokumbuka walivyokutana na Luka, tunapata taswira ya migogoro ya awali.

Anapompenda Luka, anazua mgogoro kati yake na babake, ambaye hapendelei sana ukaribu kati yao. Anahofia usalama wa bintiye. Hata hivyo, Lilia anamsisitizia kwamba mapenzi ni moja kati ya amri za Mungu wala hafai kumbagua Luka au kumwona hafai.

Hisia za Lee Imani, babake Lilia, kumhusu Luka zinazua mgogoro kati yake na nafsi yake. Japo Luka anamhakikishia kuwa nia yake kwa bintiye ni safi, hisia fulani zinamfanya kumshuku.

Hatimaye, kwa ajili ya furaha ya bintiye, analazimika kuwapa baraka zake.

Baada ya babake Lilia kufariki, ndipo migogoro inaanza kati yao. Luka anauza kanisa lao. Japo hakubaliani na hatua hii, Lilia ananyamaza ili kutunza ndoa yake. Mumewe anamwachisha kazi na kumtaka kubakia nyumbani, na hatimaye kumtawisha. Anapoingilia kampeni, anambembeleza aghairi nia lakini anakataa kabisa. Anamlazimisha Lilia kuandamana naye japo yeye hapendi masuala ya siasa. Wakati mmoja anaambulia vitisho anapokataa katakata kuandamana naye, huku akimkumbusha kuwa wanawake ni wengi.

Migogoro kati ya wawili hawa inazidi Luka anapotwaa ugavana. Anamtaka mkewe kukaa vijijini eti ili awe karibu na raia. Mumewe anafika huko wikendi wala hana wakati wake, anajiandalia masuala ya wiki inayofuata. Wakati mmoja anapomtembelea bila habari, anampata na mwanamke mwingine. Luka hajali chochote bali anamlaumu mkewe kwa kumtembelea bila taarifa. Anaporejea nyumbani jioni hiyo, anampiga vibaya mkewe na kumwonya dhidi ya kutoka nje ya nyumba.

Mafarakano yanazidi baada ya tukio hili. Luka anampiga mara kwa mara anapotangamana na majirani na marafiki. Lilia ashakuwa mtawa. Anapoamua kuripoti, anaambulia patupu baada ya kugundua mkuu wa polisi anayeenda kupigia ripoti anajuana na mumewe. Isitoshe, siku ya tatu baada ya kufika kituoni, anakosa simu ya mumewe akiwa bafuni, na hapo anajua kuwa yuko hatarini. Anangoja mumewe, ambaye anafika siku mbili baadaye.

Luka anamvamia mkewe tena na kumvuta nywele kumwelekeza kwenye chumba cha kulala, ambapo anampiga kwa ngumi, mateke na makofi. Anamvunja mkono na hatimaye anapoteza fahamu. Luka mwenyewe hajali bali anaondoka na kumwacha pale. Anahofia hata kuwaita majirani kumwauni kwa kumwogopa mumewe. Hatimaye, anaiona simu yake na kuamua kumpigia mama mkwe.

Simu ya Lilia kwa mkwewe inaibua mgogoro kati ya Luka na mamake hasa anapomjulisha ni Luka aliyetekeleza hayo. Mama mtu anashangazwa na ukatili wa Luka kwa mkewe licha ya fadhila alizotendewa na babake Lilia. Anampigia simu na kumwamrisha atume ambulansi, huku akimkumbusha kuwa akichelea, simu itakayofuata itaelekea polisi kisha kituo cha habari. Hana lingine ila kumtii mamake.

Mabadiliko- Maudhui Katika Hadithi Fupi: Mapambazuko ya Machweo

Lilia anapoelekea kwenye chumba cha kulala, anapita karibu na kioo na hapo kushuhudia mabadiliko yaliyokumba uso wake. Awali, ngozi yake ilikuwa laini bila alama yoyote na kila mara ilifanya vidu vya kupendeza alipotabasamu, tena tabasamu lenyewe halikukosa usoni mwake. Sasa hivi, uso huo umebadilika pakubwa. Ana kovu shavuni na donda linaloelekea kupona kipajini. Isitoshe, siku hizi anatabasamu kwa nadra sana.

Luka pia anakumbwa na mabadiliko. Anapokutana na Lilia mara ya kwanza, ni maskini, mchafu asiyeonekana kuwa na lolote la maana. Hata hivyo, Lee Imani anambadilisha anapomkaribisha kwake na kumpeleka shule. Anasahau umaskini na kuzidi kufana. Anaanza kufanya hata uhubiri, na hatimaye anaimarika hadi kiwango cha kuwa gavana.

Mabadiliko pia yanamkumba Luka katika sekta ya maadili. Anapomwoa Lilia, ni mhubiri na mcha Mungu mkubwa. Watu wanatoka pembe zote kufuatilia miujiza katika kanisa lake. Anawajaza wengi imani kutokana na mahubiri yake. Hata hivyo, babake Lilia anapoaga, anabadilika ghafla. Kwanza, anageuza kanisa lile kitega uchumi na kuliuza. Anawania ugavana na kuwa laghai, mzinzi na katili mkubwa asiyejali maslahi ya watu waliomchagua.

Lilia anaathiriwa zaidi na mabadiliko ya Luka. Wanapofunga pingu za maisha, maisha ni raha mstarehe kabla ya Luka kubadilika. Anamwachisha kazi na kubadili taaluma kutoka kuwa mhubiri na kujitoma katika siasa. Pia anabadilika na kuanza kumtesa mkewe. Anampiga mara kwa mara na kumwendea kinyume na vimada wengine. Anamtelekezea kijijini wala hamjali tena.

Anamchukulia kama kiumbe asiye na sauti anayefaa kuendeshwa huku na huku.

Maudhui mengine katika hadithi hii ni pamoja na Elimu, Umaskini, Kazi, Utabaka, Familia na Malezi, Ulaghai, Ubabedume, Uwajibikaji, Uongozi, Kutowajibika, Uzinzi na Kifo/Mauti.

Scroll to Top