Download All Documents- (Ksh 299) Full Day
Hurry during this Offer

Wahusika Katika Hadithi- Mapambazuko ya Machweo- Mwongozo

WAHUSIKA: Sifa na Umuhimu Lilia Katika Mapambazuko ya Machweo

Ni mwenye mapenzi ya dhati. Anapompenda Luka, anafanya kila jambo kuhakikisha amempata. Anamsisitizia babake kuwa Luka pia anastahili mapenzi. Hata anapomtesa, ananyenyekea kwake kwa imani kuwa atabadilika.

Ni mvumilivu. Mumewe anampiga kila mara na hata kumwumiza, lakini anajitia moyo huku akiomba kuwa atabadilika.

Ni mcha Mungu. Ana imani thabiti ya kidini. Anamweleza babake kuhusu amri ya Mungu ya mapenzi. Anakutana na Luka kanisani na anapokuwa mwovu, anamwombea kwa imani kuwa atabadilika.

Ni mpelelezi. Anapomweleza babake kuhusu Luka anapomwona kanisani, tunaambiwa kuwa macho yake mapelelezi hayakosi kuchunguza na ulimi wake kutangaza matokeo ya uchunguzi huo. Anafahamu kuwa mumewe ana vimada wa nje licha ya kuwa anatawishwa.

Ni mwoga. Anapomgoja mumewe, amejawa na hofu. Anaamka roho mkononi na pumzi zikimwenda mbio. Mumewe anapofika baada ya kukosa simu yake, anamfungulis huku akitetemeka kwa hofu kubwa.

Ni mpenda amani. Anafanya kila awezalo kuepuka ugomvi na mumewe. Ananyamaza anapouza kanisa. Anakatiza ukuruba na majirani kuepuka migogoro na kumwombea mumewe abadilike.

Ni msomi. Anatia bidii katika masomo yake na kufaulu katika viwango vyote hadi kufikia chuo kikuu.

Umuhimu wa Lilia

Ni kiwakilishi cha wanawake wanaokandamizwa katika jamii kwa misingi ya kijinsia.

Anadhihirisha sura tofauti za migogoro katika jamii na jinsi inavyoathiri maisha.

Kupitia kwake, madhila yanayowapata wanawake katika ndoa yanadhihirika. Ni kiwakilishi cha imani na dini na nafasi yake katika jamii

Sifa za Luka Katika Mwongozo wa Mapambazuko ya Machweo

Ni mwenye bidii. Anatia bidii katika kila afanyalo. Anapoanza kuhubiri, anachukua muda mfupi kupata umaarufu hata kumliko mhubiri mkuu. Licha ya kuzaliwa maskini, anatia bidii hadi kuwa gavana.

Ni laghai. Anajitia ucha Mungu bandia, kumbe ni mwovu kupuindukia. Anajiaminisha kwa babake Lilia. Anapokufa, anauza kanisa na kuanza kumtesa bintiye. Anajiaminisha kwa wapiga kura lakini anawapuuza wanapomchagua.

Ni mzinzi. Licha ya kuwa na mke, ana vimada wengine nje. Mkewe anapomtembelea ofisini, anampata na mwanamke mwingine ambaye ni kimada wake. Anaandamana na kimada wake katika shughuli zake huku watu wakitania kuwa ni msaidizi wake.

Ni msaliti. Anamsaliti mkewe Lilia kwa kumtesa licha ya poenzi lake la dhati. Anamsaliti babake Lilia kwa kuuza kanisa lake anapofariki na kumtesa bintiye. Anasaliti dini na nafsi kwa kubadilika kuwa mwovu.

Ni katili. Hana hata chembe cha utu. Anampiga mkewe mara kwa mara bila huruma. Anamwacha anapozirai wala hajali. Mamake anapomwamrisha kutuma ambulansi, anasita hadi anapomtishia kuripoti polisi na kumwanika kwenye kituo cha habari.

Ni mnafiki. Anajipendekeza kwa babake Lilia na kujitia wema. Anajinufaisha kwa kumwoa bintiye na kutajirika kupitia kanisa lake. Anawashawishi watu kumchagua kuwa gavana, lakini nia yake ni kujinufaisha.

Ni mwenye dharau. Anamdharau mkewe na kumdhalilisha. Anapomtembelea, anamfokea na kumwambia amwachie sekretari ujumbe. Anampiga jioni hiyo, huku akidai kuwa haheshimu wageni wake.

Ni msomi. Anakutana tena na Lilia katika chuo kikuu baada ya bidii zake katika masomo.

Umuhimu wa Luka

Ni kiwakilishi cha viongozi wanaowatelekeza wapiga kura baada ya kuwakweza mamlakani Kupitia kwake, ubabedume unadhihirika na madhara yake katika jamii

Ni kiwakilishi cha wanafiki wa kidini wanaowafumba macho wengine na kuitumia kujinufaisha Kupitia kwake, mshahara wa watenda maovu unawasilishwa kwa msomaji

Lee Imani(Babake Lilia) Mapambazuko

Ni mcha Mungu. Ni mhubiri mkuu katika kanisa. Anawalisha kondoo wa Mungu kwa neno vilivyo.

Ni mwenye mapenzi ya dhati. Anampenda mkewe kwa dhati. Tunaambiwa kuwa lau si uchangamfu wa bintiye, kumbukumbu za mkewe waliyependana kwa dhati zingemsukuma kaburini. Anashindwa kabisa kuoa tena. Pia anampenda bintiye kwa dhati.

Mwenye tahadhari. Anapogundua ukaribu kati ya Luka, anahofia madhara yake kwa bintiye na kumtuma Luka upande mwingine wa nchi kuwatenganisha. Anachelea kuwapa baraka zake kwa hisia za shauku dhidi ya Luka.

Ni mwenye utu. Anajitolea kumsaidia Luka kwa kila hali. Anamkaribisha nyumbani, kumlipia karo na hata kumpa mamake kazi.

Ni mkakamavu. Anaposhikilia lake, habadili msimamo. Anabaki pekee baada ya kifo cha mkewe.

Rai za wahubiri wengine, waumini na marafiki zake hazibadili msimamo wake.

Ni mwajibikaji. Anatekeleza wajibu wake kila mara, kama mzazi na pia mhubiri. Anawalisha chakula cha roho waumini. Anamshauri bintiye na kumpa baraka zake anapoona mapenzi yake kwa Luka.

Ni mlezi mwema. Anamlea bintiye kwa staha chini ya misingi ya kidini. Anaondokea kuwa mwenye heshima na bidii na mke mwema kwa Luka.

Umuhimu wa Lee Imani

Anawasilisha nafasi ya mzazi katika malezi na maisha ya mwanawe kwa jumla Ni kiwakilishi cha imani na dini na nafasi yake katika kujenga jamii.

Anadhihirisha matatizo yanayowakumba wazazi wanaojukumika kulea wanao peke yao. Kupitia kwake, wema miongoni mwa wanajamii unadhihirika.

Mama Luka – Sifa na Umuhimu Wake: Mapambazuko ya Machweo

Ni mwenye bidii. Anajitolea kwa kila hali kumkimu mwanawe licha ya matatizo mengi. Hatimaye anapatiwa kazi na babake Lilia kunadhifisha mazingira ya kanisa, anayoitekeleza vilivyo.

Ni mwajibikaji. Anapopokea simu ya Lilia baada ya kupigwa na Luka, anawajibika kumshughulikia kwa kumpeleka hospitalini na kumtunza. Anamshughulikia Luka pia anapolazwa humo baada ya ajali.

Ni mwerevu. Anapompigia mwanawe simu, anasita kutuma ambulensi. Anamtishia kumripoti kwa polisi na kituo cha habari, jambo linalomlazimu kumtii mara moja.

Ni mwenye utu. Anaacha shughuli zake na kumwendea mkaza mwanawe. Anampeleka hospitalini kisha kumtunza kila mara hadi anapopata afueni.

Umuhimu wake

Anawakilisha majukumu na nafasi ya mzazi katika malezi na makuzi ya mwanawe. Ni kielelezo cha wakwe wanaojali maslahi ya wakaza wanao

Anadhihirisha nafasi na umuhimu wa fadhila katika jamii.