Read Also Mwongozo Wa Bembea ya Maisha
Comprehensive Study Guide For Mapambazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine
UTANGULIZI
Mwongozo huu una nia ya kuwa mwanga gizani kwa wasomi wa diwani ya ‘Mapambazuko ya Machweo na Hadithi nyingine, kwa kutoa maelezo maridhawa kuhusiana na hadithi tofauti zilizomo humu. Ili kufanikisha hili, mwongozo huu umeangazia masuala kadhaa katika hadithi. Kabla ya kwenda katika hadithi binafsi, ni vyema kuangazia vipengele Fulani vya diwani.
MADA: Mapambazuko ya Machweo.
Mada ya diwani za hadithi fupi huwa ni mada ya mojawapo wa hadithi zilizomo. Hata hivyo, sharti iwe mada ya kuvutia wasomaji na pia yenye kubeba uzito katika diwani husika. Lnafaa kuwa mada ambayo ina uzito wa kutosha kubeba ujumbe wa diwani.
Mada ‘Mapambazuko ya Machweo’, ina athari ya kipekee kwa msomaji. Mapambazuko ni majira ya alfajiri, kabla ya jua kuchomoza hali Machweo ni wakati wa jioni, jua linapotua. Ukinzani katika mada unazua taharuki kwa msomaji, ambayo inamtuma kupitia hadithi za diwani hiyo ili kufahamu vipi Mambazuko yanatukia wakati wa Machweo.
Mada hii inaleta fikra tofauti. Kwanza, ujumbe wake unaweza kurejelea hali ya mafanikio baada ya tabu tele. Isitoshe, majira haya yananweza kurejelea umri, mapambazuko yakirejelea ujana nayo machweo uzee. Inaweza pia kumaanisha mafanikio katika machweo ya maisha(uzee).
Mada hii, hivyo basi, inabeba taarifa muhimu kwa ajili ya diwani nzima. Suala la matumaini au mafanikio katika/baada ya taabu limesawiriwa katika hadithi nyingi kwenye diwani hii. Hivyo, tunaweza kusema mada hii imefumbata ujumbe wa diwani nzima. Mifani ya hadithi zinazodhihirisha hali ya ‘Mapambazuko ya Machweo’ ni kama’Mapambazuko ya Machweo’,
‘Fadhila za Punda’, ‘Toba ya Kalia’, ‘Nipe Nafasi’,
‘Ahadi ni Deni’, ‘Sabina’ na nyinginezo.
Hivyo basi, ni wazi kwamba mada ‘Mapambazuko ya Machweo’ inafaa kabisa kwa diwani hii.
JALADA:– Mwongozo Wa Mapambazuko
Jalada katika diwani ya hadithi fupi aghalabu hubeba ujumbe wa hadithi iliyobeba anwani. Hali si tofauti katika diwani hii. Jalada linaakisi hali katika hadithi ya ‘Mapambazuko ya Machweo.
Kuna bwana aliyevaa suti ambaye anaingia kwenye gari. Haikosi huyo ni Makutwa, anayemiliki gari la kibinafsi pekee mjini Kazakamba.
Kando yake, kuna mwanamume na mwanamke wanaoonekana kuwa katika hali ya majibizano kwa jinsi walivyoinua mikono, mwanamume mkono wa kulia na mwnamke mkono wa kushoto nyuso zikielekeana. Hawa bila shaka ni Makucha na mkewe Macheo ambao wana mjadala mara kwa mara kuhusiana na suala la Makutwa kumkebehi Makucha.
Kando ya wawili hao pembeni kulia, kuna kimeza kidogo chenye vifaa fulani na kiti chake. Haikosi hapo ni sehemu anapouzia vitafunio Makucha. Pembeni kulia kulia nako kuna sehemu ya nyumba, ambayo itakuwa ya Makucha na mkewe Macheo.
Mbele yao mbali kidogo, kuna watoto wadogo wanaoonekana kuwa katika shughuli za kuzoa mchanga. Hawa ni watoto ambao Makutwa anawatumikisha katika mgodi wake kinyume cha sheria.
Hali ya anga inadhihirisha kwamba ni wakati wa machweo. Kuna jua ambalo linaelekea kutua na anga imetamalaki rangi ya samawati. Mchanga walikokanyaga wahusika wote unatuhakikishia ni mandhari ya mji wa Kazakamba.
Kuutumia Mwongozo– Wa Mapambazuko
Mwongozo huu umechambua kila hadithi kwa mapana na marefu. Umeangazia masuala tofauti tofauti katika hadithi zote, ili kuhakikisha kwamba maomaji anaelewa yanayoshughulikiwa kwa ubainifu wa kipekee. Masuala haya yanaanzia kwa mtiririko wa hadithi na ufaafu wa anwani hadi mitindo ya uandishi. Masuala yaliyoshughulikiwa ni pamoja na;
Dhamira ya Mwandishi.
Ni lengo la mwandishi, yaani sababu ya kuandika hadithi husika. Inaeleza ujumbe ambao mwandishi alinuia kupitisha kwa msomaji. Inaweza pia kuelezwa kama mafunzo ambayo msomaji anapata kutokana na kusoma hadithi husika. Dhamira inaweza kuwa kupitisha ujumbe kwa njia tofauti ikiwemo kuonya, kusawiri hali Fulani katika jamii au kuelimisha kuhusu suala fulani.
Maudhui
Ni masuala nyeti yanayoshughulikiwa katika hadithi. Ni mambo makuu hasa kuhusu jamii yanayoibuka kutokana na kusoma hadithi Fulani. Baadhi ya maudhui yanayojitokeza katika hadithi nyingi ni pamoja na elimu, utamaduni, mapenzi na ndoa, migogoro na migongano, uzinzi, ulaghai na unafiki, usaliti, nafasi ya mwanamke, ubabaedume na mengi mengine.
Wahusika
Ni watu au viumbe ambao wanatumiwa na mwandishi kuwasilisha ujumbe wake kwa hadhira. Katika hadithi zote, wahusika waliotumika ni binadamu, wanaoakisi jamii halisi. Wahusika hawa hutofautiana kwa hulka(sifa) kulingana na ujumbe toofauti ambao mwandishi anawatumia kupitisha. Hivyo basi, kila mhusika, wahusika wakuu na wasaidizi huwa na sifa zake na umuhimu katika hadithi.
Mbinu za Uandishi.
Ili kuleta mvuto, mwandishi hawezi kutumia lugha iliyo kavu. Lazima aifinyange lugha na kuisuka kipekee ili kuleta mnato kwa msomaji anapoanza kupitia kazi yake. Kuna aina tofauti za mitindo ya uandishi ambayo hutumika kutimiza hili.
1. ISTILAHI ZA LUGHA/ TAMATHALI ZA USEMI Katika Mwongozo Wa Mapambazuko
Tashbihi/Tashbiha/Mshabaha. Hii ni mbinu ya kufananisha vitu viwili vyenye sifa sawa kwa kutumia vihusishi vya ulinganisho kama vile mithili ya, kama, sawasawa na, mfano wa na nyinginezo. Kwa mfano; Kamau ni mrefu mithili ya twiga.
Istiara/Sitiari. Hii ni mbinu ya kulinganisha vitu viwili vyenye sifa sawa moja kwa moja bila kutumia vihusishi vyovyote. Kwa mfano; Siku hizi amekuwa wali wa daku(yaani ameadimika, haonekani)
Tashihisi/Uhuishi/Uhaishaji. Ni mbinu ya kuvipa sifa za uhai vitu visivyo na uhai kama vile kuongea, kutangamana na kutekeleza mambo ya kibinadamu. Kwa mfano; hofu ilimkumbatia.
Methali. Ni tungo fupi zilizogawika katika sehemu mbili ambazo hubeba ujumbe wenye hekima. Huwa na maana ya juu, inayotokana na maneno yaliyotumiwa na maana ya ndani isiyohusiana na maneno hayo, ambayo huongoza matumizi yake. Kwa mfano; mla na miwili hana mwisho mwema.
Semi(Misemo na Nahau). Ni tungo fupi zinaoundwa kwa kuunganisha maneno, na ambazo maana yake na matumizi huwa tofauti na maneno yaliyotumika. Kwa mfano; enda segemnege- haribika, enda kombo.
Takriri/ Uradidi. Ni mbinu ya kurudiarudia neno au fungu la maneno kwa nia ya kutilia mkazo hoja fulani au kusisitiza. Uradidi huu unawea kutumiwa na mwandishi moja kwa moja katika usimulizi au ukatumiwa na mhusika katika mazungumzo. Kwa mfano;misitu kwa misitu ya mahindi na maharagwe.
Tabaini. Ni mbinu ya kutumia ukinzani kwa nia ya kudhihirisha wingi. Aghalabu hudhihirika kwa
matumizi ya ‘si’ ya ukanushi. Kwa mfano; kila kitu kwake kilipendeza, si macho, si uso, si
mavazi, si viatu, si sauti.
Chuku. Ni matumizi ya maelezo yaliyotiliwa chumvi kwa ajili ya kuonyesha uzito wa jambo au hoja fulani, na pia kumtumbuiza msomaji. Maelezo huelezwa kwa kiasi cha kuchekesha, kwani huzua hali ambazo ni wazi haziwezekani, lakini zinazokubalika kifasihi. Kwa mfano; hasira zake zingeweza kuivunja bilauri kwa kuiangalia tu.
Balagha/Maswali Balagha. Ni mbinu ya kutumia maswali yasiyohitaji majibu, kwa kuwa aidha majibu yako wazi, hayapo au hayahitajiki. Maswali haya husaidia kuelewa fikra za mhusika, kutoa taarifa zaidi au kumchochea msomaji kuwaza zaidi. Kwa mfano; kwa nini haya yanipate mimi?
Uzungumzi Nafsia/Monolojia. Ni mbinu ambapo mhusika hujizungumzia mwenyewe aidha kwa sauti au akilini. Huwezesha msomaji kujua mawazo, maoni au mipango ya mhusika. Kwa mfano;
“Muradi haya yashatokea, sina budi kukubali,” Mercy alijisemea moyoni.
Tanakali/ Tanakali za Sauti. Ni mbinu ya kuiga milio au sauti zinazotokea katika hali tofauti za kimazingira au sauti za wanyama na vitu tofauti. Kwa mfano; kriii! Kriii! Kriii! Simu yangu ilikiriza.
Dayolojia. Ni mbinu ya kutumia mawasiliano ya moja kwa moja kati ya wahusika wawili katika usemi halisi. Mawasiliano haya huhusu mada fulani wanayochangia wote. Mbinu hii busaidia kuonyesha mkinzano wa kimawazo, migogoro, maoni gofauti ya wahusika, n.k.
Kuchanganya Ndimi/ Lugha Mseto. Hii ni mbinu ya kutumia lugha mbili tofauti katika usemi, Kiswahili na lugha nyingine. Mara nyingi, maneno kutoka lugha ya pili huandikwa kwa mtindo wa italiki. Aghalabu huwa Kiingereza lakini yaweza kuwa lugha nyingine kama lugha ya mama,
Kiarabu, n.k. kwa mfano; “Mwanao ni mzima. He’s out of danger.”
Utohozi. Ni matumizi ya maneno kutoka lugha nyingine, aghalabu Kiingereza yaliyobadilishwa muundo na matamshi kuwa ya Kiswahili. Kwa mfano. Daktari(doctor), begi(bag), ticket(tiketi),n.k
Kejeli/ Stihizai/ Dhihaka. Ni mbinu ya kutumia maneno ya kumsimanga mtu, tukio au suala fulani. Hali hii huweza kupunguza uzito wa hali au jambo au kumtilia mtu hamu ya kubadilika. Inaweza kutumiwa na mwandishi mwenyewe katika maelezo ya suala au mhusika kwa mwingine. Kwa mfano; alipata alama 10 katika hisabati. Kweli alijaribu, kama binadamu.
Nidaa. Ni mbinu ya kudhihirisha hisia za ndani kwa kutumia vihusishi na alama ya hisi(!). Kwa mfano, alifurahi sana kufika nyumbani. Popote ambapo alama hiyo imetumika, hiyo ni mbinu ya nidaa. Mtihani mkuu kwa mwanafunzi ni kufahamu hisia ambazo zinaakisiwa na alama hiyo.
Zinaweza kuwa furaha, huzuni, mshangao, mtamauko, hasira, amri, n.k. Laiti angalijua!
Koja. Ni mbinu ya kudhihirisha wingi wa vitu kwa matumizi ya koma kwa ajili ya kuorodhesha. Mbinu hii inaweza kuwasilisha kuwepo kwa lukuki ya vitu au mfuatano wa matukio mengi. Kwa mfano; Maria alifika nyumbani, akavua sare za shule, akaoga, akaenda mtoni kuchota maji, akapika, akala na kulala.
Mdokezo. Ni mbinu ya kuachia mambo yakining’inia, yaani kuacha bila kukamilisha ujumbe fulani kwa kutumia alama za dukuduku(…). Inaweza kuwa sehemu inayoweza kujazwa, itakayoelezwa mbeleni au kumwachia msomaji kujijazia. Pia inaweza kuwa zao la kukatizwa kalima wakati wa mazungumzo. Kwa mfano; aliingia ndani na kusubiri akijua wazi kuwa mgaagaa na upwa…
Tasfida. Ni mbinu ya kutumia msamiati wenye adabu ili kuepuka lugha chafu. Hutumika kuepuka lugha inayoweza kuzua hisia hasi au kutia kinyaa. Kwa mfano, mja mzito badala ya kuwa na mimba, kubaua/kutabawali au kwenda haja ndogo badala ya kukojoa.
Tadmini. Ni mbinu ya kutoa marejeleo katika misahafu(vitabu vya kidini) kama vile Biblia na Korani, na kuyahusisha na hali fulani katika kazi ya kifasihi. Kwa mfano; ukaidi haujaanza leo, ulianza na Adamu na Hawa kwenye bustani la Edeni.
Tanakuzi. Ni mbinu ya kutumia maneno yenye kinyume katika sentensi moja na kuzua kauli zenye ukinzani. Aghalabu hutumika kuonyesha hali ya utata. Kwa mfano; asali iligeuka shubiri. Alikufa na kufufuka ilipobidi.
Lahaja. Ni matumizi ya maneno ya lahaja tofauti za Kiswahili ambayo hayapo katika Kiswahili sanifu. Upekee wake ni matumizi ya maneno yasiyo ya Kiswahili sanifu bali vilugha vyake. Kwa mfano; kahawa tungu(kahawa chungu), mwananti kuivunda nti(mwananchi kuivunja nchi).
2. Mbinu za Kimtindo Mwongozo Wa Mapambazuko
Sadfa. Ni mtindo ambapo matukio mawili yanayohusiana hutukia kibahati kwa wakati mmoja, au kwa mfululizo kama kwamba yamepangwa. Matukio haya aghalabu huwa na matokeo fulani.
Kwa mfano; kukutana na msaada wakati wa tatizo bila kutarajia.
Kinaya. Ni mtindo ambapo matukio huenda kinyume na matarajio yetu, aidha kulingana na mfululizo wa awali wa matukio, au kwa kuyalinganisha na maisha halisi. Pia mbinu hii inaweza kudhihirishwa kupitia kwa usemi wa mhusika. Kwa mfano; kumpa hongera mtu aliyefeli au kusherehekea baada ya kufeli.
Majazi. Ni mtindo wa kuwapa wahusika majina kulingana na tabia au maumbile yao. Majina haya huitwa majina ya majazi/kimajazi. Kwa mfano; mtu katili anaweza kupatiwa jina ‘Kedi’.
Taswira. Mtindo wa kutoa maelezo ya ndani kuhusu suala fulani kiasi cha kujenga picha ya kile kinachorejelewa kwenye akili ya msomaji. Kuna taswira toofauti kama vile mwonekano, mnuso au harufu, hisi na mguso, kulingana na picha inayozalishwa. Kwa mfano; kaptura yake nyeusi iliyochakaa ilirembwa kwa viraka vya kila rangi, hungetambua rangi yake asilia.
Taharuki. Ni mtindo wa kutoa maelezo taratibu kwa kusaza habari fulani ili kumtia msomaji hamu ya kujua zaidi. Pia huweza kumwacha msomaji akining’inia mwishoni mwa kisa na kumwacha kujijazia kuhusu masuala fulani.
Kisengerenyuma/Mbinu Rejeshi. Ni mtindo wa kurejelea matukio yaliyotukia muda uliopita, lakini yenye uhusiano na yale yanayosimuliwa. Yanaweza kurejeshwa na msimulizi au mhusika fulani kupitia kumbukumbu zake.
Kiangaza Mbele/Kisengerembele/Kionambele. Ni mtindo wa kudokeza mambo yatayotukia mbele kabla hayajatukia, na kuyahusisha na yale yanayotukia wakati huo.
Utabiri. Ni mbinu ambapo mhusika hudokeza jambo kisha likatukia baadaye bila yeye kutarajia. Tofauti yake na Kiangazambele ni kwamba utabiri huwa jambo la kukisia au kudokeza tu, bila uhakika wake wa kutokea.
Jazanda. Ni ufananisho wa mzito wa vitu viwili visivyo na uhusiano wa moja kwa moja, ambavyo hulinganishwa na kulinganuliwa kwa njia ya mafumbo. Kwa mfano, Bi. Sarafu alilalamika kuwa jembe la mumewe lilishindwa na kazi.
Ishara. Ni mambo, vitu au matukio ambayo huonekana au kutukia kabla ya jambo fulani yanayoashiria. Mambo haya huwa na uhusiano fulani na matukio yanayoashiria. Kwa mfano; milio ya bundi inayomtia mhusika wasiwasi kabla ya janga fulani kutokea.
Ritifaa. Ni mtindo ambapo mhusika aliye hai humzungumzia mhusika aliyefariki kama kwamba yuko hai na anamsikia. Huweza kuonyesha uhusiano kati yao, kueleza hisia za ukiwa au kumtakia neema.
Lakabu. Ni matumizi ya majina ya kupanga kuwarejelea wahusika. Majina haya huambatana na sifa fulani za mhusika. Tofauti na majazi ni kuwa lakabu huwa majina ya kupanga, bali si majina halisi ya wahusika.
Ushairi Nyimbo. Barua
Mwingiliano wa Vipengele Katika Mwongozo Wa Mapambazuko
Ni muhimu kuelewa kwamba kuna mwingiliano wa kipekee katika vipengele hivi tofauti vya hadithi, kwani haviwezi kushughulikiwa kwa ukamilifu. Baadhi ya mwingiliano ni kama ufuatao;
Dhamira ya Mwandishi na Maudhui. Dhamira ndiyo huongoza maudhui ambayo yanashughulikiwa katika hadithi. Hivyo basi, mambo haya mawili huingiliana pakubwa. Dhamira ndiyo hufungua nafasi kwa maudhui ya hadithi. Kwa mfano, iwapo mwandishi anadhamiria kudhihirisha maovu yanayotendewa wananchi na wanasiasa au viongozi, lazima kuwepo maudhui ya siasa au uongozi au yote.
Dhamira na Wahusika. Kila dhamira huwasilishwa kwa kutumia mhusika au wahusika fulani. Bila wahusika, dhamira haiwezi kutimizwa wala wahusika hawawezi kuwa na maana bila dhamira. Sifa za wahusika zinalingana na dhamira na kubwa zaidi, umuhimu wao huhusiana moja kwa moja na dhamira ambayo wanatekeleza. Kwa mfano, iwapo mwandishi anadhamiria kudhihirisha madhila ya wanawake katika jamii, lazima awepo mwanamke anayetekeleza dhima hiyo.
3. Maudhui na Wahusika Katika Mapambazuko
Maudhui huwasilishwa kupitia kwa wahusika pia. Vitendo vya wahusika ndivyo huzalishwa maudhui yanayoangaziwa katika hadithi. Hivyo basi, kuna uhusiano mkubwa kati ya sifa za wahusika na maudhui. Kwa mfano, kukiwepo na maudhui ya usaliti, lazima kuwepo mhusika msaliti, iwapo kuna maudhui ya tamaa na ubinafsi, lazima kuwepo mhusika mbinafsi na mwenye tamaa. Hivyo basi, ni vyema msomaji kuoanisha masuala haya pale ambapo hayashughulikiwa yote mawili.
Maudhui na Mtindo/Mbinu za Uandishi. Kuna pia mwingiliano wa kadri kati ya vipengele hivi. Japo si kila mara haya hutokea, baadhi ya mbinu huingiliana na Maudhui. Baadhi ya mbinu husawiri maudhui fulani. Kwa mfano, mtindo wa kinaya aghalabu huhusiana pakubwa na maudhui ya usaliti. Mbinu tofauti pia hubeba maudhui mengine kama vile dayolojia, ushairi, nyimbo, n.k.
Mtindo na Wahusika. Mitindo pia huweza kusaidia kuelewa wahusika na hulka zao zaidi. Kwa mfano, mbinu za majazi na lakabu husaidia katika kuelewa sifa za wahusika fulani. Mbinu nyingine zinazoleta haya ni kama dayolojia, kinaya, uzungumzi nafsia na nyinginezo.
Kutokana na maelezo haya, ni muhimu kutilia maanani kila ujumbe unaopatikana kwenye hadithi zote ili kuimarisha uelewa wake na pia kuwa na uwezo wa kukabiliana nazo katika mtihani.
1.Fadhila za Punda- Rachel Wangari. Mtiririko
Lilia anagutuka kutoka usingizini kwa hofu. Anamsubiri mumewe Luka. Amelala kochini ili amfungulie haraka. Anagundua kwamba bado hajafika kama alivyodhania, lakini hili halimpunguzii hofu, kwani ana hakika kuwa atakuja tu, tena kwa hasira tele kwa kukosa kupokea simu yake, ambayo ilipigwa akiwa bafuni. Ni saa nane za usiku na watu wamelala.
Anafahamu kuwa mumewe haji na kuamua kuelekea kitandani kulala. Anapita kwenye kioo kilichopasuka, tokeo la pigo moja la awali la mumewe. Anajiona alivyobadilika, kovu shavuni na donda linaloelekea kupona kipajini. Anakumbuka uso wake awali ulivyokuwa laini na wa kupendeza, na kushangaa hasa sababu ya Luka, mumewe, kubadilika na kuwa mkali hivi. Hatimaye analala.
Tunarejeshwa awali, Lilia alipomwona Luka mara ya kwanza, katika kanisa la babake, alipoingia ghafla tu. Alilazimika kukaa karibu na Lilia kwa kuwa ndipo palikuwa na nafasi. Alivaa mavazi ya kimaskini, lakini alipoomba kuimba, aliisikia sauti yake iliyokuwa tamu ajabu, iliyompendeza hata babake Lilia.
Babake Lilia ni mjane kwa miaka mitatu, lakini kila mara Lilia anamwondolea mawazo ya marehemu mkewe, kwanza kwa jinsi wanavyofanana na pia kwa ule ulimi wake usiotulia. Anamweleza kuhusu Luka na sauti yake yake ya kipekee. Anapomsumbua kuhusu kijana huyo, anaamua kumwalika ofisini Jumapili inayofuata. Mhubiri anajuta kuchelewa kupata mtoto mwingine kabla ya mkewe kufariki kwa ajali.
Shinikizo la kuoa tena haliridhii, kwani haoni yeyote anayeweza kujaza pengo la mkewe.
Anampa mamake Luka kazi ya kusafisha kanisa, naye Luka anajiunga na shule ya msingi kwa hisani ya mhubiri. Anaondokea kuwa mwerevu. Urafiki wake na Lilia unamtia mchungaji kiwewe, na hivyo anamtuma Luka kwa mhubiri rafikiye upande mwingine wa nchi. Urafiki wao haukatishwi na hili.
Wanazidi kuwasiliana kwa simu na barua. Wanakutana tena katika chuo kikuu kimoja. Baba anamwonya bintiye lakini hamsikizi kutokana na mapenzi.
Lilia anamkumbusha babake kuhusu amri ya Mungu ya mapenzi. Luka anamsisitizia kuwa ana nia safi kwa mwanawe na ataka kumuoa. Japo hisia fulani zinamfanya kutomwamini Luka, hana ushahidi na pia hataki kumvunja moyo bintiye. Anawapa Baraka zake. Wakati huu Lilia ni meneja wa benki moja. Luka anaongoza mahubiri kanisani kutokana na uzee wa baba Lilia, mhubiri mkuu. Kanisa linakua na kufurika hadi mahema kuongezwa.
Baba Lilia anafariki na Luka kuchukua uongozi kamili wa kanisa. Anamshinikiza mkewe kuacha kazi ili atunze fedha za kanisa, japo kuna mhasibu anayefanya kazi nzuri. Anamtaka kukaa nyumbani na kuandamana naye anapohitajika. Umaarufu wa Luka unazidi hadi anafika ikulu.
Luka anaamua kuingilia siasa japo mkewe hapendezwi. Anauza kanisa, lakini Lilia ananyamaza kulinda ndoa. Kampeni zanamchosha Lilia hadi siku moja anapokataa kabisa kushiriki, akiwa na uja uzito wa miezi mine. Luka anaudhika na kuondoka nyumbani. Jioni ya siku inayofuata, anapelekwa hosppitalini na majirani na kupoteza uja uzito. Luka hahuzuniki sana, kwa kuwa hataki kuwa mzazi wakati wa uchaguzi.
Luka anafaulu kuwa gavana lakini anawasahau wananchi. Anakuwa mzinzi. Anapohamia kasri la gavana, anamsahau mkewe na kumtaka kubaki vijijini ili awe karibu na raia. Anamtembelea mkewe wikendi.
Anapata taarifa kuwa mumewe ana vimada, lakini haamini hadi anapomtembelea ofisini bila habari na kumpata na mwanamke mwingine. Wanazozana na kuamrishwa arudi nyumbani, jambo analotii. Jioni hiyo, Lilia anapigwa na kuonywa vikali dhidi ya kwenda ofisi bila idhini ya mumewe. Hatimaye anaishia kutawishwa, haongei na watu kwa hofu ya kupigwa. Anamwona mumewe akiandamana na yule mwanamke aliyepata ofisini, anayetaniwa kuwa mshauri wake.
Wakati mmoja anaamua kuripoti polisi. Anapofika, anapelekwa kwa mkuu wa kituo. Mkuu huyu anaposifia ukarimu wa mumewe waliyekuwa pamoja wiki jana, anajua kuwa hatasaidika. Anadanganya kuwa anamtafuta askari polisi aliyemfaa siku moja na kujiendea. Anatoka kwa hofu akijua Luka ataambiwa. Siku mbili zikapita, kisha siku ya tatu ndipo akakosa kupokea simu yake, naye Luka akakosa kufika.
Luka anafika siku tano baada yake kutembelea kituo cha polisi na kumpiga vibaya hadi anapopoteza fahamu na kutoweka. Anaiona simu yak chini na kuichukua, na kumpigia mama mkwe na kuzirai tena. Anapopata fahamu, yuko mikononi mwa mama mkwe anayemhudumia. Anamlaani Luka kwa anayomtendea mkewe licha ya fadhila za baba Lilia kwake. Anampigia Luka kumwamrisha atume ambulensi, akimtishia kupiga simu polisi na kituo cha habari. Anakata na kuendelea kumshughulikia mkaza mwanawe. Kabla ya fahamu kumtoka, Lilia anasikia mlio wa ambulensi.
Anapogutuka, anajipata peke yake kitandani kwenye chumba cha hospitali. Mama mkwe anamtembelea kila siku kumuunguza, wala hajamwona mumewe. Siku ya nne, anamwona mtu kando yake, hamtambui kwani amefungwa bendeji usoni, nao mguu umeinuliwa. Mama mkwe anapokuja, anaelekea kwa kile kitanda. Akija, anawahudumia wote wawili. Anamrejelea kuwa gavana, lakini Lilia haelewi ni gavana yupi na kwa nini wamo chumba kimoja, naye mama mkwe hana nia ya kumweleza.
Mgonjwa mwenzake anaanza kutembelewa na marafiki na wafanyakazi waliokunja nyuso. Anawasikia wauguzi wakisema huenda asitembee tena kutokana na ajali aliyopata, ambayo nusura imwangamize. Lilia anaelewa mambo siku ya nne, mama mkwe anapofika na kumwita mgonjwa kwa jina, Luka!
Anamweleza kuwa kiruukanjia wake aliondoka baada ya kusikia hawezi kutembea tena. Lilia naye ameruhusiwa kwenda nyumbani. Anapomwangalia mumewe, anadhani anaona chozi likitoka kwenye jicho la kushoto ambalo halijafungwa bandeji.
Ufaafu wa anwani ‘Fadhila za Punda’. Mwongozo Wa Mapambazuko
Anwani hii inatokana na methali isemayo, ‘Fadhila za punda ni mashuzi’, kama ilivyotumiwa katika hadithi yenyewe. Pia huweza kuwa ‘Fadhila za punda ni mateke’. Matumizi ni kwa ambaye hulipa hisani kwa nuksani, yaani wema kwa uovu. Fadhila za punda, hivyo basi, ina maana ya matendo mabaya kutoka kwa mtu aliyetendewa mema. Mada hii inaafiki hadithi.
Luka ana fadhila za punda. Kwanza, kanisa ambalo linamlea na kumjenga akiwa maskini anaponeemeka analiuza bila kujali. Umaarufu na utajiri anaopata hapa unamtia kiburi sana.
Luka analipa fadhila za Lilia kwa mashuzi. Lilia ndiye anampigania kwa mhubiri hadi anaposaidiwa kimaisha na kimasomo, akasoma hadi chuo kikuu.
Lilia vile vile anapigania penzi lake kwa Luka kwa kila hali. Anatia bidii kuhakikisha mapenzi yao yanadumu kila babake anapojaribu kuwatenganisha. Hata maonyo ya baba mtu hayamfanyi kubadili msimamo. Hatimaye wanaruhusiwa kuoana.
Licha ya haya yote, anamtesa Lilia katika ndoa yao kwa kipigo cha kila mara kutokana na visingizio vya hapa na pale, kama vile chakula kukosa chumvi ya kutosha na kuchelewa kumfungulia. Anamtia makovu katika uso uliokuwa mzuri na mwororo awali.
Licha ya kutopenda siasa, Lilia anamsaidia Luka katika azma yake ya kuwa gavana hadi anapofaulu. Hata hivyo, anamdhalilisha na kumtelekeza anapotwaa wadhifa huo na kutomjali kabisa.
Lilia anampenda mumewe kwa dhati ya moyo na yuko tayari kufanya kila awezalo kulinda ndoa yake. Anaridhia matakwa ya Luka na kuwa mwaminifu kwake. Luka kwa upande wake, badala ya kulipa fadhila hizi kwa kuwa mume mwema, ana vimada wa pembeni wal hafanyi lolote kumficha mkewe ukweli huu.
Baba Lilia anamtendea Luka mengi. Anafadhili elimu yake na kumlea kama mwanawe na hatimaye kumkubalia kumwoa bintiye. Anapofanikiwa baadaye, anaanza kumtesa bintiye aliyeahidi kumtunza.
Luka anpiga kampeni kabambe katika azma ya kuwa gavana, nao wananchi wanamuunga mkono. Anapofanikiwa, halipii fadhila zao kwani anawasahau kabisa, wala dhiki yao haimshtui.
Kimada wake Luka pia anakejeli fadhila za Luka. Anamzuzua na kumfanya kumsahau kabisa mkewe wa ndoa. Anaandamana naye kila mahali akiwa gavana. Anapopata ajali na kulazwa hospitali, kimada huyu anamtoroka baada ya kusikia hawezi kutembea tena.
Dhamira ya Mwandishi Wa Mapambazuko
Kuonya dhidi ya kuwaamini waja wanaojitia ucha Mungu, kwani unaweza kuwa bandia. Ucha Mungu si kilemba cheupe tu. Ni vyema kufanya uchunguzi wa ndani kabla ya kumwamini yeyote.
Anadhamiria kutoa ushauri kuhusiana na nafasi ya mzazi katika makuzi ya mwanawe au wanawe na jinsi ya kutekeleza malezi kwa tija.
Ananuia pia kutoa maonyo kwa viongozi wasiowajibikia wajibu wao wanapotwikwa mamlaka kuwa siku yao itafika.
Kuonya watenda maovu kuwa siku ya kuyalipia itakuja, kwani malipo ni hapa hapa duniani.
Kuonya dhidi ya uvumilivu usio na tija katika ndoa za dhuluma ambao unaweza kuleta madhara yasiyomithilika kwa wahusika.
Kudhihirisha jinsi mwanamke anavyodhulumiwa katika jamii na jinsi anavyoweza kukabili na kupinga dhuluma hizi.
Kuonyesha sura za migogoro katika jamii na jinsi zinavyoathiri maisha.
Maudhui Ya Mapenzi na Ndoa Katika Mapambazuko
Mapenzi ndiyo chemchemi inayochangia ndoa. Kuna ndoa ya babake Lilia ambayo ilitawaliwa na mapenzi, kwani wakati huu mkewe ashaaga. Kila mara mhubiri huyu anamkumbuka. Hata anashindwa kuoa mke mwingine kutokana na mapenzi yao ya dhati. Anapatwa na huzuni tele baada ya kuaga kutokana na ajali ya barabarani. Mwandishi anasema kuwa lau si ulimi wa bintiye usiotulia, dhiki ya kuachwa na mkewe ingemsukuma kaburini. Fahari kuu ya ndoa inadhihirika kupitia kujaliwa kwao binti huyu, Lilia, ambaye anfanana na mamake.
Ndoa kuu, hata hivyo, ni kati ya Luka na Lilia. Mapenzi yao yanaanza Lilia anapomwona Luka kwenye kanisa la babake, huku amevalia kimaskini. Sauti yake tamu inamvutia mara moja na hapo haachi kumwaza. Mapenzi yake kwa Luka yanamsukuma kumwomba babake amsaidie.
Babake anampeleka katika shule ya msingi na kumpa mamake kazi ya kusafisha kanisa.
Anamwelimisha hadi chuo kikuu, yote kwa ajili ya bintiye anayempenda Luka kwa dhati.
Usuhuba kati ya wawili hawa unaanza mapema, tangu wakiwa wachanga. Unamtia kiwewe babake Lilia, ambaye anajaribu kila mbinu kuwatenganisha bila mafanikio. Anapompeleka Luka upande mwingine wa nchi kwa mhubiri mwenzake, bado wanawasiliana kwa barua na simu. Bintiye anamsisitizia amri ya Mungu ya mapenzi na kumtaka awape baraka zake. Licha ya hisia za hofu kwa Luka, anawaruhusu kuoana.
Ndoa yao inaenda vizuri hadi babake Lilia anapofariki. Hapo Luka anabadilika na kuwa mwovu. Anamshinikiza mkewe kuacha kazi na kumtawisha. Hatimaye anaamua kujitosa katika siasa na mkewe anatakiwa kuwajibika, licha ya kuwa hapendi siasa. Anapokataa kushirikiana naye baada ya muda, anamkumbusha kuwa wanawake ni wengi na kumwacha pekee nyumbani. Analazimika kukimbizwa hospitalini na majirani na anapoteza uja uzito wake wa miezi minne, lakini Luka hahuzuniki sana.
Anaamini bado upo muda wa kupata watoto.
Mambo yao yanaharibika kabisa Luka anapokuwa gavana. Anaanza kuwa na vimada, huku akimlazimisha mkewe kuishi vijijini ili awe karibu na raia. Anamtembelea wikendi lakini hana muda naye, shughuli muhimu kwake ni kujiandaa kwa ajili ya wiki inayofuata. Mkewe anapomtembelea bila habari na kumpata na mwanamke mwingine, hajali chochote bali anamfokea mkewe na kumtaka arejee nyumbani na kuacha ujumbe Jioni hiyo anaporudi nyumbani, Luka anampiga mkewe vibaya, huku akimkanya dhidi ya kufika ofisini kwake bila taarifa na kutoheshimu wageni wake. Huu unaondokea kuwa mwanzo wa vipigo vya mara kwa mara. Ata kuhusiana na marafiki na majirani ananyimwa. Mumewe anaandamana na yule kimada wake katika hafla zote bila haya.
Lilia anaamua kuripoti polisi lakini anaghairi anapogundua mkuu wa polisi anajuana na mumewe. Anahofia usalama wake kutokana na kisa hicho, akijua mumewe atajua, pamoja na kukosa simu yake akiwa bafuni. Hofu yake inaondokea kuwa ukweli, kwani Luka anaporejea, anampiga vibaya hadi anapozirai na kumwacha. Anapopata fahamu, anamwita mama mkwe anayemwauni kwa kumpeleka hospitali. Hata haamini Luka anaweza kumfanyia Lilia hivi!
Haibainiki ndoa ya Luka inachukua mkondo gani mwishowe. Mkewe anatibiwa na kuruhusiwa kuondoka hospitalini, hali Luka mwenyewe amelazwa baada ya kupata ajali. Kimada wake naye amemtoroka baada ya kusikia huenda asiweze kutembea tena maishani.
Nafasi ya Mwanamke Katika Jamii. Mwongozo Wa Mapambazuko
Mwanamke katika jamii hii amepatiwa nafasi finyu sana, licha ya kuwa na mchango wa kipekee. Kwanza, mwanamke anadhihirika kuwa mpenzi wa dhati ya moyo. Mhubiri anamkumbuka mkewe waliyependana kwa dhati na ambaye anapofariki, anashindwa kabisa kuoa mke mwingine wa kujaza
pengo lake. Anashinikizwa na wahubiri wenzake, wazee wa kanisa na hata washirika wake lakini anashindwa kabisa kumwoa mwingine.
Lilia anapomwona Luka mara ya kwanza tu, anampenda kwa dhati hasa kutokana na sauti yake ya kupendeza. Anamshinikiza babake hadi anapompa mamake kazi ya kusafisha kanisa na hata kumpeleka Luka shule. Majaribio ya babake kuwatenganisha hayazai matunda kwani Lilia yuko mstari wa mbele kumpigania Luka wake hadi wanaporuhusiwa kuoana na baba kuwapa baraka zake.
Hata Luka anapoingilia siasa, Lilia anamsaidia licha ya kutopenda siasa. Anamvumilia na ukware wake na kubaki kuwa mwaminifu siku zote. Anampiga mara kwa mara, lakini anazidi kumshughulikia kama mumewe hadi anampiga na kumsababisha kulazwa hospitalini.
Wanakutana huko baada ya Luka kupata ajali ya barabarani na kupoteza uwezo wa kutembea. Hatujui ndoa yao inachukua mkondo gani.
Mamake Luka pia ana mapenzi ya kipekee. Anampenda mwanawe Luka na anajitolea kumlea vyema licha ya umaskini wake. Lilia anapopoteza fahamu baada ya kipigo, anachukua simu na kumpigia. Anafika mara moja na kumhudumia. Anampigia mwanawe na kumlazimisha kutuma ambulensi, kisha kumpeleka Lilia hospitalini na kumuuguza.
Mwanamke pia anachukuliwa kama kiumbe dhaifu cha kuendeshwa na kuelekezwa na mwanamume. Luka anampa mkewe maagizo anayotaka kila mara. Anamkataza kujumuika na marafiki na anapofanya hivyo anampiga vibaya. Anamlazimisha kukaa nyumbani kama mtawa na kumtaka kumpigia simu akitaka kufika ofisini. Anapokosa simu yake akioga, anaingiwa na hofu kuu, kwani anajua yatakayofuatia. Luka anampiga mara kwa mara hadi mwisho anapolazwa hospitalini.
Mwanamke pia anasawiriwa kama chombo cha kumstarehesha mwanamume. Luka anamwambia mkewe kuwa wanawake ni wengi anapokataa kuandamana naye katika kampeni. Kulingana naye, ni rahisi kwake kupata wanawake wengine. Anapokuwa gavana, ana vimada wengi wala hajali hili linavyomwathiri mkewe. Anapomtembelea anampata na mwanamke mwingine. Badala ya kuwa na haya anamfokea na kumlaumu. Mwanamke yule naye pia anaendelea kuhusiana na Luka kimapenzi licha ya kujua ana mke.
Mwanamke pia anachorwa kama msaliti. Kimada wa Luka anajua kuwa ana mke lakini bado anasuhubiana naye na hata kuandamana naye katika shughuli rasmi. Hajali machungu anayomletea mkewe Luka. Isitoshe, anamtoroka Luka anapomhitaji zaidi, pale anapopata ajali na kupoteza uwezo wa kutembea.
USALITI Katika Mapambazuko
Luka anamsaliti babake Lilia. Mzee huyu anajitolea kumfaa kwa kila hali tangu akiwa mchanga. Anamsomesha na kumpa uongozi wa mahubiri katika kanisa lake. Anapofariki, anauza kanisa lake kwa nia ya kujifaidi binafsi. Pia anamsaliti kwa kuvunja ahadi aliyotoa ya kumlinda bintiye, kwani baada ya kumwoa anaanza kumtesa.
Luka pia anamsaliti mkewe Lilia. Kwanza, anamsaliti kwa kumwendea kinyume licha ya uvumilivu wa madhila ya mumewe na pia uaminifu wake. Pia, mkewe anapigania penzi tangu wakiwa wachanga. Anamshinda hata babake anayemshuku Luka. Licha ya haya yote, Luka anamtesa kwa mapigo ya kila siku hadi mwishowe anapolazwa hospitalini kwa mapigo haya.
Luka pia anasaliti dini na imani kwa kutumia kanisa kwa ajili ya manufaa ya kibinafsi. Kanisa linakua na kuimarika chini ya mahubiri yake, lakini linapokua, analigeuza biashara. Hatimaye analiuza na kuingilia siasa. Anasaliti dini na Imani pia kwa kubadilika na kuwa laghai, mkware, dhalimu miongoni mwa maovu mengine.
Kimada wa Luka anamsaliti kwa kumwacha anapomhitaji zaidi. Licha ya kumtelekeza mkewe kwa sababu ya kimada huyu, anamwacha kwenye kitanda cha hospitali anapopoteza uwezo wake wa kutembea.
Isitoshe, anamsaliti Lilia kwa kuhusiana na mumewe akijua vyema amemwoa.
Dini
Jamii hii imejikita katika dini ya kikristo. Dini inachukua mkondo wake wa kuwapa waja tumaini na kuwatia shime. Dini pia inasaidie walio katika taabu kuwa na tumaini la maisha.
Lilia anakutana na Luka mara ya kwanza katika kanisa. Wako katika darasa la mabaleghe anapofika. Sadfa kuwa ni pale alipokaa tu Lilia penye nafasi anaiona kama ni Mungu anamjaribu. Anaketi na masomo kuendelea. Mwishoni mwa somo anapatiwa nafasi ya kujitambulisha. Anamtukuza Mungu kwa wimbo unaowapendeza waliomo humu, hata mhubiri anayekuja kuwajulisha muda umekwisha.
Lilia pia amelelewa katika misingi ya kikristo, kwani babake, Lee Imani ni mhubiri. Anamlea pekee baada ya mkewe kuaga kutokana na ajali ya barabarani.
Dini ndiyo inayopalilia penzi kati ya Luka na Lilia. Lilia anamwomba babake wamsaidie Luka kama dini inavyoelekeza. Babake anakubali kumpeleka shule na pia kumpa mamake kazi ya kusafisha kanisa.
Wanapojuana wakiwa watoto, Luka na Lilia ni marafiki wa kufa kuzikana. Wanapoingia ujanani, babake Lilia anahofia usalama wa bintiye na kujaribu kuwatenganisha kwa kumpeleka Luka upande mwingine wa nchi kwa mhubiri rafikiye. Bado wanawasiliana kwa simu na barua.
Mhubiri huyu anapotilia shaka mwelekeo wa uhusiano wa bintiye na Luka, bintiye anamkumbusha mahubiri yake mwenyewe kila mara kuwa Mungu ni upendo. Anamwambia kuwa hafai kumbagua Luka au kuona kama hamfai. Lee Imani analazimika kumuuliza Luka kuhusu nia yake kwa Lilia, naye anasisitiza kuwa ana nia safi kabisa. Licha ya mashaka aliyo nayo, hana lingine ila kuwapa Baraka zake.
Lilia anamshawishi babake kumpa Luka jukumu la kuhubiri kanisani, jukumu ambalo anatekeleza vilivyo. Anahubiri na baada ya muda, kanisa linafurika hadi mahema kuongezewa. Washirika wanampenda sana. Watu wanatoka nchi za mbali kufuatilia miujiza huku.
Lee anapofariki, Luka anageuza kanisa kuwa kitega uchumi. Anamwachisha mkewe kazi yake ya umeneja wa benki ili aje kutunza pesa za kanisa, japo kuna mhasibu anayefanya kazi vizuri. Baada ya muda, anauza kanisa lile na kuingilia siasa. Anasahau kabisa mambo ya dini na kubadilika kabisa. Anawatenga watu waliomchagua, anamtesa mkewe na kuwa mkware kupindukia. Mkewe naye anaishi kumwombea kwa imani kuwa atabadilika siku moja.
Migogoro
Mwanzo wa hadithi unadhihirisha mgogoro mkuu katika kisa hiki. Lilia yuko katika hali ya wasiwasi mkuu huku akimsubiri mumewe. Amezoea vitimbi vya mumewe anayemjia kwa makeke kila siku. Anapopita karibu na kioo akielekea kwenye chumba cha kulala, mabadiliko katika uso wake yanadhihirisha
migogoro ya awali kati yake na mumewe. Kwanza, kioo chenyewe kimepasuka. Ana kovu shavuni na donda linaloelekea kupona shavuni, zote kumbukumbu za mapigo ya awali.
Lilia anapokumbuka walivyokutana na Luka, tunapata taswira ya migogoro ya awali.
Anapompenda Luka, anazua mgogoro kati yake na babake, ambaye hapendelei sana ukaribu kati yao. Anahofia usalama wa bintiye. Hata hivyo, Lilia anamsisitizia kwamba mapenzi ni moja kati ya amri za Mungu wala hafai kumbagua Luka au kumwona hafai.
Hisia za Lee Imani, babake Lilia, kumhusu Luka zinazua mgogoro kati yake na nafsi yake. Japo Luka anamhakikishia kuwa nia yake kwa bintiye ni safi, hisia fulani zinamfanya kumshuku.
Hatimaye, kwa ajili ya furaha ya bintiye, analazimika kuwapa baraka zake.
Baada ya babake Lilia kufariki, ndipo migogoro inaanza kati yao. Luka anauza kanisa lao. Japo hakubaliani na hatua hii, Lilia ananyamaza ili kutunza ndoa yake. Mumewe anamwachisha kazi na kumtaka kubakia nyumbani, na hatimaye kumtawisha. Anapoingilia kampeni, anambembeleza aghairi nia lakini anakataa kabisa. Anamlazimisha Lilia kuandamana naye japo yeye hapendi masuala ya siasa. Wakati mmoja anaambulia vitisho anapokataa katakata kuandamana naye, huku akimkumbusha kuwa wanawake ni wengi.
Migogoro kati ya wawili hawa inazidi Luka anapotwaa ugavana. Anamtaka mkewe kukaa vijijini eti ili awe karibu na raia. Mumewe anafika huko wikendi wala hana wakati wake, anajiandalia masuala ya wiki inayofuata. Wakati mmoja anapomtembelea bila habari, anampata na mwanamke mwingine. Luka hajali chochote bali anamlaumu mkewe kwa kumtembelea bila taarifa. Anaporejea nyumbani jioni hiyo, anampiga vibaya mkewe na kumwonya dhidi ya kutoka nje ya nyumba.
Mafarakano yanazidi baada ya tukio hili. Luka anampiga mara kwa mara anapotangamana na majirani na marafiki. Lilia ashakuwa mtawa. Anapoamua kuripoti, anaambulia patupu baada ya kugundua mkuu wa polisi anayeenda kupigia ripoti anajuana na mumewe. Isitoshe, siku ya tatu baada ya kufika kituoni, anakosa simu ya mumewe akiwa bafuni, na hapo anajua kuwa yuko hatarini. Anangoja mumewe, ambaye anafika siku mbili baadaye.
Luka anamvamia mkewe tena na kumvuta nywele kumwelekeza kwenye chumba cha kulala, ambapo anampiga kwa ngumi, mateke na makofi. Anamvunja mkono na hatimaye anapoteza fahamu. Luka mwenyewe hajali bali anaondoka na kumwacha pale. Anahofia hata kuwaita majirani kumwauni kwa kumwogopa mumewe. Hatimaye, anaiona simu yake na kuamua kumpigia mama mkwe.
Simu ya Lilia kwa mkwewe inaibua mgogoro kati ya Luka na mamake hasa anapomjulisha ni Luka aliyetekeleza hayo. Mama mtu anashangazwa na ukatili wa Luka kwa mkewe licha ya fadhila alizotendewa na babake Lilia. Anampigia simu na kumwamrisha atume ambulansi, huku akimkumbusha kuwa akichelea, simu itakayofuata itaelekea polisi kisha kituo cha habari. Hana lingine ila kumtii mamake.
Mabadiliko
Lilia anapoelekea kwenye chumba cha kulala, anapita karibu na kioo na hapo kushuhudia mabadiliko yaliyokumba uso wake. Awali, ngozi yake ilikuwa laini bila alama yoyote na kila mara ilifanya vidu vya kupendeza alipotabasamu, tena tabasamu lenyewe halikukosa usoni mwake. Sasa hivi, uso huo umebadilika pakubwa. Ana kovu shavuni na donda linaloelekea kupona kipajini. Isitoshe, siku hizi anatabasamu kwa nadra sana.
Luka pia anakumbwa na mabadiliko. Anapokutana na Lilia mara ya kwanza, ni maskini, mchafu asiyeonekana kuwa na lolote la maana. Hata hivyo, Lee Imani anambadilisha anapomkaribisha kwake na kumpeleka shule. Anasahau umaskini na kuzidi kufana. Anaanza kufanya hata uhubiri, na hatimaye anaimarika hadi kiwango cha kuwa gavana.
Mabadiliko pia yanamkumba Luka katika sekta ya maadili. Anapomwoa Lilia, ni mhubiri na mcha Mungu mkubwa. Watu wanatoka pembe zote kufuatilia miujiza katika kanisa lake. Anawajaza wengi imani kutokana na mahubiri yake. Hata hivyo, babake Lilia anapoaga, anabadilika ghafla. Kwanza, anageuza kanisa lile kitega uchumi na kuliuza. Anawania ugavana na kuwa laghai, mzinzi na katili mkubwa asiyejali maslahi ya watu waliomchagua.
Lilia anaathiriwa zaidi na mabadiliko ya Luka. Wanapofunga pingu za maisha, maisha ni raha mstarehe kabla ya Luka kubadilika. Anamwachisha kazi na kubadili taaluma kutoka kuwa mhubiri na kujitoma katika siasa. Pia anabadilika na kuanza kumtesa mkewe. Anampiga mara kwa mara na kumwendea kinyume na vimada wengine. Anamtelekezea kijijini wala hamjali tena.
Anamchukulia kama kiumbe asiye na sauti anayefaa kuendeshwa huku na huku.
Maudhui mengine katika hadithi hii ni pamoja na Elimu, Umaskini, Kazi, Utabaka, Familia na Malezi, Ulaghai, Ubabedume, Uwajibikaji, Uongozi, Kutowajibika, Uzinzi na Kifo/Mauti.
WAHUSIKA: Sifa na Umuhimu Lilia
Ni mwenye mapenzi ya dhati. Anapompenda Luka, anafanya kila jambo kuhakikisha amempata. Anamsisitizia babake kuwa Luka pia anastahili mapenzi. Hata anapomtesa, ananyenyekea kwake kwa imani kuwa atabadilika.
Ni mvumilivu. Mumewe anampiga kila mara na hata kumwumiza, lakini anajitia moyo huku akiomba kuwa atabadilika.
Ni mcha Mungu. Ana imani thabiti ya kidini. Anamweleza babake kuhusu amri ya Mungu ya mapenzi. Anakutana na Luka kanisani na anapokuwa mwovu, anamwombea kwa imani kuwa atabadilika.
Ni mpelelezi. Anapomweleza babake kuhusu Luka anapomwona kanisani, tunaambiwa kuwa macho yake mapelelezi hayakosi kuchunguza na ulimi wake kutangaza matokeo ya uchunguzi huo. Anafahamu kuwa mumewe ana vimada wa nje licha ya kuwa anatawishwa.
Ni mwoga. Anapomgoja mumewe, amejawa na hofu. Anaamka roho mkononi na pumzi zikimwenda mbio. Mumewe anapofika baada ya kukosa simu yake, anamfungulis huku akitetemeka kwa hofu kubwa.
Ni mpenda amani. Anafanya kila awezalo kuepuka ugomvi na mumewe. Ananyamaza anapouza kanisa. Anakatiza ukuruba na majirani kuepuka migogoro na kumwombea mumewe abadilike.
Ni msomi. Anatia bidii katika masomo yake na kufaulu katika viwango vyote hadi kufikia chuo kikuu.
Umuhimu wa Lilia
Ni kiwakilishi cha wanawake wanaokandamizwa katika jamii kwa misingi ya kijinsia.
Anadhihirisha sura tofauti za migogoro katika jamii na jinsi inavyoathiri maisha.
Kupitia kwake, madhila yanayowapata wanawake katika ndoa yanadhihirika. Ni kiwakilishi cha imani na dini na nafasi yake katika jamii
Luka
Ni mwenye bidii. Anatia bidii katika kila afanyalo. Anapoanza kuhubiri, anachukua muda mfupi kupata umaarufu hata kumliko mhubiri mkuu. Licha ya kuzaliwa maskini, anatia bidii hadi kuwa gavana.
Ni laghai. Anajitia ucha Mungu bandia, kumbe ni mwovu kupuindukia. Anajiaminisha kwa babake Lilia. Anapokufa, anauza kanisa na kuanza kumtesa bintiye. Anajiaminisha kwa wapiga kura lakini anawapuuza wanapomchagua.
Ni mzinzi. Licha ya kuwa na mke, ana vimada wengine nje. Mkewe anapomtembelea ofisini, anampata na mwanamke mwingine ambaye ni kimada wake. Anaandamana na kimada wake katika shughuli zake huku watu wakitania kuwa ni msaidizi wake.
Ni msaliti. Anamsaliti mkewe Lilia kwa kumtesa licha ya poenzi lake la dhati. Anamsaliti babake Lilia kwa kuuza kanisa lake anapofariki na kumtesa bintiye. Anasaliti dini na nafsi kwa kubadilika kuwa mwovu.
Ni katili. Hana hata chembe cha utu. Anampiga mkewe mara kwa mara bila huruma. Anamwacha anapozirai wala hajali. Mamake anapomwamrisha kutuma ambulansi, anasita hadi anapomtishia kuripoti polisi na kumwanika kwenye kituo cha habari.
Ni mnafiki. Anajipendekeza kwa babake Lilia na kujitia wema. Anajinufaisha kwa kumwoa bintiye na kutajirika kupitia kanisa lake. Anawashawishi watu kumchagua kuwa gavana, lakini nia yake ni kujinufaisha.
Ni mwenye dharau. Anamdharau mkewe na kumdhalilisha. Anapomtembelea, anamfokea na kumwambia amwachie sekretari ujumbe. Anampiga jioni hiyo, huku akidai kuwa haheshimu wageni wake.
Ni msomi. Anakutana tena na Lilia katika chuo kikuu baada ya bidii zake katika masomo.
Umuhimu wa Luka
Ni kiwakilishi cha viongozi wanaowatelekeza wapiga kura baada ya kuwakweza mamlakani Kupitia kwake, ubabedume unadhihirika na madhara yake katika jamii
Ni kiwakilishi cha wanafiki wa kidini wanaowafumba macho wengine na kuitumia kujinufaisha Kupitia kwake, mshahara wa watenda maovu unawasilishwa kwa msomaji
Lee Imani(Babake Lilia)
Ni mcha Mungu. Ni mhubiri mkuu katika kanisa. Anawalisha kondoo wa Mungu kwa neno vilivyo.
Ni mwenye mapenzi ya dhati. Anampenda mkewe kwa dhati. Tunaambiwa kuwa lau si uchangamfu wa bintiye, kumbukumbu za mkewe waliyependana kwa dhati zingemsukuma kaburini. Anashindwa kabisa kuoa tena. Pia anampenda bintiye kwa dhati.
Mwenye tahadhari. Anapogundua ukaribu kati ya Luka, anahofia madhara yake kwa bintiye na kumtuma Luka upande mwingine wa nchi kuwatenganisha. Anachelea kuwapa baraka zake kwa hisia za shauku dhidi ya Luka.
Ni mwenye utu. Anajitolea kumsaidia Luka kwa kila hali. Anamkaribisha nyumbani, kumlipia karo na hata kumpa mamake kazi.
Ni mkakamavu. Anaposhikilia lake, habadili msimamo. Anabaki pekee baada ya kifo cha mkewe.
Rai za wahubiri wengine, waumini na marafiki zake hazibadili msimamo wake.
Ni mwajibikaji. Anatekeleza wajibu wake kila mara, kama mzazi na pia mhubiri. Anawalisha chakula cha roho waumini. Anamshauri bintiye na kumpa baraka zake anapoona mapenzi yake kwa Luka.
Ni mlezi mwema. Anamlea bintiye kwa staha chini ya misingi ya kidini. Anaondokea kuwa mwenye heshima na bidii na mke mwema kwa Luka.
Umuhimu wa Lee Imani
Anawasilisha nafasi ya mzazi katika malezi na maisha ya mwanawe kwa jumla Ni kiwakilishi cha imani na dini na nafasi yake katika kujenga jamii.
Anadhihirisha matatizo yanayowakumba wazazi wanaojukumika kulea wanao peke yao. Kupitia kwake, wema miongoni mwa wanajamii unadhihirika.
Mama Luka.
Ni mwenye bidii. Anajitolea kwa kila hali kumkimu mwanawe licha ya matatizo mengi. Hatimaye anapatiwa kazi na babake Lilia kunadhifisha mazingira ya kanisa, anayoitekeleza vilivyo.
Ni mwajibikaji. Anapopokea simu ya Lilia baada ya kupigwa na Luka, anawajibika kumshughulikia kwa kumpeleka hospitalini na kumtunza. Anamshughulikia Luka pia anapolazwa humo baada ya ajali.
Ni mwerevu. Anapompigia mwanawe simu, anasita kutuma ambulensi. Anamtishia kumripoti kwa polisi na kituo cha habari, jambo linalomlazimu kumtii mara moja.
Ni mwenye utu. Anaacha shughuli zake na kumwendea mkaza mwanawe. Anampeleka hospitalini kisha kumtunza kila mara hadi anapopata afueni.
Umuhimu wake
Anawakilisha majukumu na nafasi ya mzazi katika malezi na makuzi ya mwanawe. Ni kielelezo cha wakwe wanaojali maslahi ya wakaza wanao
Anadhihirisha nafasi na umuhimu wa fadhila katika jamii.
Mbinu za Uandishi Tashbihi
Atakuja tu, labda ghamidha itakuwa imezidi, imefura kama hamuri lililotiwa hamira. Sasa kucheka kwake kulikuwa nadra kama kupatwa kwa mwezi.
Swali likajitunga akilini mwake, na kama mwangwi, likawa linajirudia tena na tena. Shati lenyewe limekuwa mararu, limemganda kama kigaga.
Watoto waliokuwa na hamu kutoka nje wakawa watulivu kana kwamba viti vimekuwa sumaku. Wamefika nusu safari, bintiye katulia kama maji mtungini.
Sasa kazi kukilea kitoto chao, kibinti hiki kilichomlanda mamake kama shilingi kwa ya pili. Badala yake liliuchochea, kama moto kuvuvia.
Nia yangu nyeupe kama pamba.
Sasa mumewe anataka kujisiriba uchafu ule na kama mchezea tope, atarukiwa tu. Ona umbo lako sasa, kama nguruwe.
Kisha kofi likaandamwa na teke lililomlaza kochini kama zigo lililosukumwa likajiangukia ovyo. Ilikuwa kama kuchokoza nyuki.
Lilia alimfungulia mlango akitetemeka kama unyasi upepo uvumapo.
Tashihisi
Saa ukutani ilimwambia saa nane za usiku,
Fikra zimechoka, mwenyewe hajiwezi; nusura yake usingizi uliomsomba, ukampa utulivu, japo wa muda tu.
Kama si ulimi wa bintiye ambaye hatulii, kihoro kingemvamia labda hata kumvuta kuelekea kaburini. Lakini hawakujua ajali ya barabara ingeyafuta maisha ya mama mtu. Nguo zilezile, usafi bado unampiga chenga. Lakini dhiki ziliwaandama.
Istiara
Isije ikawa mwenye nyumba kaja na yeye mpangaji akachelewa kumfungulia mlango. Mbona Luka akageuka kuwa mzigo wa moto, habebeki, habebeki kamwe?
Yamekolezwa ladha na sauti, asali kando.
Akatamani kufika nyumbani apumzike, kazi ya kuwalisha kondoo wa Mungu si kazi rahisi.
Lilia, malaika wake, hampi utulivu wa kuwazia sana kuhusu upweke wake. Naye wembe masomoni, akili zake sumaku, hunasa yote wafunzayo walimu. Kaloa, katota hili penzi la jogoo la mji.
Na ule ulimi wake uliodondoka asali, waumini wakampenda. Kwake siasa ni mchezo mchafu.
Lilia akatambua rangi halisi ya mumewe. Tamaa ndiyo ibada yake, Ulaghai sasa ndiyo ibada yake kubwa, mhubiri keshakuwa mhadaifu.
Ulimfanya mkeo ngoma kwa sababu ya hawara ambaye hakuthamini hata chembe.
Semi na Nahau roho mkononi, pumzi zikimwenda mbio- yaani kwa wasiwasi tele. nyanyaso moto mmoja- yaani
tele, zisizokoma.
hakuwa na budi- alilazimika, hakuwa na lingine yalikuwa yale yanayodaiwa kumtoa nyoka pangoni- yalivutia sana akawa hoi- akachoka sana.
kufunga pingu za maisha- kuoana. unampiga chenga- unamhepa rafiki yake wa kufa kuzikana- rafiki mkubwa/wa dhati.
binti hasikii la mwadhini wala la mteka maji msikitini- hasikii lolote wala yeyote. kumvunja
moyo- kumuumiza hisia. wakafunga pingu za maisha- wakaoana. Lilia alipigwa na butwaa- alishangaa alipokataa katakata-
alipokataa kabisa. kumuunga mkono- kumsaidia kutimiza azma yake, kukubaliana naye. hajali habali- hajali hata kidogo, hajali chochote. utajua kilichomtoa kanga manyoya shingoni- utaingia mashakani/utaumia. Akamkaribisha kwa
mikono miwili- akamkaribisha vizuri, kwa ukuruba mzuri. amepata nafuu- hali yake imeimarika/ afya yake imeimarika aage dunia- afariki, akufe.
Kisengerenyuma/Mbinu Rejeshi
Lilia anapopita karibu na kioo, anaona mabadiliko usoni mwake; kovu na donda linaloelekea kupona. Yanamkumbusha vita vya awali vya mumewe, na sura yake ya zamani.
Anakumbuka alipokutana na Luka kanisani, akampenda na kumsihi babake wamsaidie. Wakaenda shule pamoja hadi wakaoana na babake kuaga, huku akimwachia Luka usukani wa kanisa.
Anakumbuka mabadiliko ya Luka baada ya babake kuaga; kuuza kanisa na kuanza kumdhulumu.
Akaingilia siasa licha ya kujaribu kumshawishi, na kutwaa ugavana, kisha akageuka katili.
Anakumbuka zaidi hatua yake ya kumripoti ilivyotibuka baada ya kugundua mkuu wa kituo ni rafiki ya mumewe, na wasiwasi uliompata akijua mumewe ataambiwa.
Lilia anapofika katika kituo cha polisi, mkuu wa kituo anamweleza kuwa alikuwa na mumewe Lilia siku iliyotangulia katika hoteli moja.
Mama Luka anapompeleka Lilia hospitali, anashangaa vipi Luka amesahau fadhila alizofanyiwa na babake Lilia.
Mamake Luka anamkumbusha alivyomgeuza mkewe ngoma kwa ajili ya kimada asiyemjali. Alimweleza kuwa alikuja siku ya kwanza kumwona, kisha siku ya pili akageuka na kuondoka aliposikia hawezi kutembea tena.
Maswali Balagha
Mbona ikawa hivi? Mbona Luka akageuka kuwa mzigo wa moto, habebeki, habebeki kamwe? Nitapata wapi mwandani kama mke wangu marehemu?
Afanye nini baba mtu?
Chuo kimoja, bahati gani hii?
Mume wako? Tena lipi haliwezi kusubiri hadi mwisho wa juma? Je, huyu mwenzangu kapiga simu naye?
Bwana gavana, uko hapa?
Gavana yupi huyu na mbona wako chumba kimoja?
Siku nne wamekuwa chumba kimoja na mumewe na hana habari?
Yu wapi yule kirukanjia wako? Wajua yuko wapi? … waona sasa? Atakutunza nani? Atakuuguza nani, maana kwako fadhila za punda ni mashuzi!
Taharuki.
Kisa kinapoanza, tunaachwa na maswali mengi. Tunashangaa ni nani haswa Lilia anayengoja na kwa nini anamwogopa kiasi hicho. Kumbukumbu zake zinatujibu baadaye.
Baada ya masimulizi kuhusu matukio ya awali katika maisha ya Lilia, ni wazi kwamba mumewe atamtesa akirejea. Tunabaki na hamu kubwa ya kujua tendo atakalofanya akirejea baada ya mkewe kukosa simu yake na kujaribu kumripoti polisi.
Lilia anapoamka na kupata mtu mwinine kalazwa kando yake, hajui ni nani. Tunabaki na hamu ya kujua ni nani hadi mama mkwe anapoeleza baadaye, ndipo tunafahamu ni Luka.
Mwisho wa hadithi pia unatuacha na maswali mengi. Hatujui maisha ya Luka yanachukua mkondo gani baada ya kupoteza uwezo wa kutembea, hatujui iwapo mkewe atamtunza, hatujui iwapo atabakia kuwa gavana. Hatujui kama mienendo yake itabadilika au atabakia katili alivyo.
Kinaya
Tunaambiwa kuwa Lilia ana tabia za kiutu uzima wala hana marafiki wa umri wake. Ni ajabu kwa kuwa aghalabu watu huwa na marafiki wa umri wao.
Babake Lilia anawatenganisha Luka na bintiye ili kukatiza urafiki wao. Badala yake, tendo hili linachochea zaidi urafiki huo.
Luka anamwachisha mkewe kazi kwa madai ya kumtaka kudhibiti pesa za kanisa. Kinaya ni kuwa bado yupo mhasibu wa kanisa anayefanya kazi nzuri.
Luka anamtaka mkewe kuandamana naye katika kampeni ili watu waone kiongozi anayethamini ndoa na familia. Ukweli ni kuwa hamthamini mkewe wala familia. Hata mkewe kupoteza mimba si hoja kwake.
Luka anampiga mkewe kwa kumtembelea bila habari akidai anamwaibisha na kuwafanya wapinzani wake kusema ameshindwa kudhibiti mkewe, sembuse kaunti nzima. Ukweli ni kuwa Luka anajiaibisha mwenyewe kwa vitendo vyake, na kaunti imemshinda kudhibiti.
Lilia anapomwuliza mumewe kuhusu mwanamke wanayeandamana, anapokea kichapo, huku Luka akimwonya kuwa akichezea ukarimu wake atajipata nje akiombaomba. Ukarimu wake si ukarimu.
Methali
Mvumilivu hula mbivu.
Usione wembamba wa reli ukashangaa garimoshi kupita pale. Mstakabali wa binadamu ni usiku wa giza
Yaliyopita si ndwele Umdhaniaye ndiye kumbe siye Kuro haisemi uongo Lisemwalo lipo, kama halipo li njiani laja. Mwanzo wa ngoma ni lele
Fadhila za punda ni mashuzi Uliacha mbachao kwa msala upitao Taswira
Sura ya Lilia anapojitazama kiooni na ile ya awali; “kovu shavuni, donda linaloelekea kupona kipajini. Alikumbuka sura aliyozoea kuiona. Lile kovu shavuni halikuwepo, badala yake ngozi nyororo,
iliyojishobwekea na vidu kudhihiri kila alipocheka.”
Luka anapoingia kanisani mara ya kwanza. “Nywele zilikuwa matimutimu, uso umechora mistari mieupe… Shati refu limemfika magotini, upande mmoja halikuchomekwa kiunoni. Shati lenyewe
lilikuwa mararu, limemganda mwilini kama kigaga. Suruali fupi ambayo uzi umetokeza kiunoni, bila huo uzi
ingejidondokea.”
Kipigo cha kwanza cha Lilia; “Jioni ile alipofungua mlango…,alipokezwa kofi ambalo lilimfanya kuona vimulimuli. Kisha kofi likaandamwa na teke lililomlaza kochini…”
Taswira ya kipigo kinachomlaza hospitali; “Lilia alimfungulia mlango akitetemeka kama unyasi upepo uvumapo. Mara akashikwa nywele, karibu zing’oke. Kisha akabururwa hadi kwenye chumba cha malazi. Si kipigo hicho. Si makofi, si ngumi, si mateke, tena ya mtu aliyevaa buti.”
Tabaini
Si bughudha hizo, nyanyaso moto mmoja.
Si utamu wa maneno huo! Ni yale yanayodaiwa kumtoa nyoka pangoni.
Si wahubiri wenza, si wazee wa kanisa, si washiriki, waote walimtaka kuoa tena… Na si kichapo hicho alichochapwa.
Si makofi, si ngumi, si mateke, tena ya mtu aliyevaa buti.
Tanakali za Sauti Alitega sikio ndi! Chumba cheupe pe!
Lilia alikuwa amelala fofofo,
Mwongozo Wa Mapambazuko ya Machweo
Sadfa
Anapoelekea kwenye chumba cha kulala, Lilia anasadifu kupita mkabala na kioo, na hapo anayaona mabadiliko ya sura yake.
Luka anapoingia kanisani, inasadifu kuwa nafasi iliyo wazi ni pale tu alipoketi Lilia, hivyo analazimika kuketi naye. Pia, mjo wake unasadifiana na funzo linaloendelea kuhusu kumpenda jirani, Lilia anauona mjo huo kama mtihani kutoka kwa Mungu kuhusu funzo hilo.
Luka anapowasilisha wimbo wake, inatokea sadfa kuwa mhubiri ndio anakuja kuwataarifu muda umekwisha, na hapo anaisikia sauti yake tamu.
Babake Lilia anafanya kila juhudi kuwatenganisha Lilia na Luka. Sadfa inawakutanisha tena wanapohudhuria chuo kikuu kimoja.
Inasadifu kuwa Lilia anapomtembelea Luka ofisini mwake bila taarifa, kimada wake pia amefika, hali inayozua mtafaruku kati yao.
Lilia anapofika kuripoti mumewe, anaitiwa mkuu wa polisi. Inasadifu kuwa mkuu huyo anajuana na mumewe, na hata walikuwa pamoja siku iliyotangulia.
Lilia anapogutuka baada ya kuzirai kutokana na kipigo cha mumewe, hajui amwite nani kwani mumewe anamkataza kuwa na urafiki na majirani. Kisadfa, anaiona simu yake chini ya kitanda na anapoibonyeza, nambari anayokutana nayo kwanza ni ya mama mkwe.
Lilia na mumewe wanakutana hospitalini kisadfa. Lilia akiuguza majeraha ya kupigwa naye, Luka anahusika kwenye ajali na kuletwa pale pale alipolazwa Lilia.
Majazi
Lilia. Anamlilia babake hadi anapokubali kumsaidia Luka. Analilia ndoa yake Luka anapobadilika na kuanza kumpiga. Anamlilia Mungu kwa maombi ambadilishe mumewe. Anapopigwa na kuzirai, anachukua simu na kumlilia mkwewe.
Imani. Jina la babake Lilia. Anawajaza watu imani katika dini kwa kuwa yeye ni mhubiri. Licha ya shauku yake kwa Luka, anamruhusu kumwoa Lilia akiwa na imani wataishi vyema.
Anamsaidia Luka kupata elimu na hata kumpa mamake kazi.
Luka. Ni jina la mmojawapo wa waandishi wa Biblia na wahubiri wa injili ya Yesu. Kabla ya kuingiwa na uovu, Luka ni mhubiri mzuri mwenye waumini wengi na anayefahamika sana. Watu wanatoka pembe zote kuja kupokea miujiza kwake.
Mbinu nyingine ni kama vile Utohozi, Lakabu, Kejeli, Nidaa, Takriri, Dayolojia, Kuchanganya Ndimi, Chuku na Uzungumzi Nafsia.
2. Msiba wa Kujitakia- D. W. Lutomia Mtiririko wa hadithi
Wakazi wa Matopeni wako katika kipindi kigumu sana cha maisha, taabu zinawaandama kila uchao wala hawana wa kumlilia. Machoka ni mmoja kati ya Wasakatonge wanaoishi mtaa wa matopeni. Amefika nyumbani jioni akitoka katika shughuli za kutafuta kibarua ili kupata cha kutia tumboni lakini hajaambulia chochote. Anaona tofauti kubwa iliyopo kati ya wapiga kura na wale wanaopigiwa kura.
Hali yake inamkumbusha shairi alilowahi kusoma, la ‘Msiba wa Kujitakia’, ambao kamwe hauna kilio. Ndio hali waliyo nayo baada ya kuwachagua viongozi wasiojali maslahi yao. Anakumbuka wakati wa siasa kabla ya uchaguzi. Serikali inajinaki jinsi ilivyoleta maendeleo huku upinzani nao ukipuuzilia mbali hoja hizo. Wanatoa ahadi tele za kuboresha maisha ya wakazi wa mtaa huu.
Machoka anakumbuka kauli ya jirani yake, Zuhura kuwa wanafaa kumchagua mtu wa ukoo wao, awe anafaa au la, tendo ambalo hata Zuhura mwenyewe anajutia. Tofauti kati ya uteuzi wao wa viongozi
uliwafanya kuzua uadui, lakini sasa dhiki inawaleta pamoja. ‘Mtu wake’ aliyechagua Zuhura
hawafai kitu. Bidhaa zinapanda bei na maisha kuwa magumu. Anagundua kosa lake.
Wakati wa uchaguzi, jimbo la Matopeni linageuzwa ngome ya watu fulani. Wananchi wanarauka mapema kwenda kupiga kura kwa matumaini kuwa viongozi hao wataboresha maisha yao. Hata hivyo, wanawatelekeza. Zuhura anakumbuka akimweleza Machoka walivyokosea kwa kumchagua kiongozi kwa kuwa ni wa ukoo wao, au kutokana na vizawadi vidogo vidogo walivyopatiwa na visenti vya kununulia pombe. Hali inazidi kuwa ngumu kwa wakazi wa Matopeni. Udhalimu unazidi, huku mapato yao madogo yakimegwa na ushuru.
Fumo Matata ni mpinzani mkuu wa Sugu Junior. Anawakumbusha wapiga kura kukoma kupigia viongozi kura kwa kuwa ni wa ukoo wao kwani hali hiyo inawaathiri. Kauli yake haitiliwi maanani. Fumo mwenyewe anawania kiti hiki kwa mara ya tatu mfululizo.
Ni miaka arobaini na mitatu tangu jimbo la Matopeni likombolewe kutoka kwa walowezi kwa uongozi wa Sugu Senior, babake Sugu Junior. Zuzu Matata, babake Fumo Matata alipendelewa na wakoloni kuongoza lakini akakataa akiwataka kumwachilia kwanza Mzee Sugu Senior kutoka gerezani.
Alipoachiliwa, akawa na umaarufu kumshinda na kutwaa uongozi kwa shuruti za wazee wa jamii yake. Hali hii ikazua uhasama kati yao hadi Zuzu Matata alipofariki bila kuongoza jimbo hili. Mwanawe pia anazidi kupambana kutimiza ndoto hiyo. Ni familia hizi mbili tu zinazozozania uongozi wa Matopeni.
Fumo Matata anapigiwa upatu kushinda ila mambo yanabadilika. Matokeo yanapokuja, Sugu Junior ameshinda licha ya Fumo kuwa na wafuasi wengi na kupiga kampeni ya kupigiwa mfano. Yasemekana kuwa upigaji kura si hoja, kwani katika kuzihesabu, mambo huenda kombo na wananchi kulimbikiziwa viongozi wasiowataka.
Fumo Matata anapata ujumbe kutoka kwa mwandani wake, Kahindi Mlalama, akimpongeza kwa
‘ushindi’. Hata hivyo, anamwonya kuwa ushindi huo huenda usione jua, lakini siku zijazo uchaguzi
utakuwa huru na wa haki, bali si wa kulimbikiziwa viongozi madikteta na wakoloni mamboleo.
Vipimo vya uongozi vitategemea sera na tajriba bali si ukoo, umaarufu au utajiri.
Kiwanjani Mamboleo, shughuli ya kumwapisha Sugu Junior inaandaliwa. Saa tatu asubuhi, watu washafika huku wanahabari wakinasa matukio yanayopeperushwa moja kwa moja. Wapo viongozi wa majimbo mengine, mawaziri, wabunge na viongozi tofauti serikalini. Sherehe bila shaka imegharimu mamilioni ya pesa za watoaushuru kama kina Machoka na Zuhura. Yasemekana serikali ndiyo imegharamia nauli ya ndege ya viongozi wa majimbo mengine kutokana nao kutilia shaka ushindi wake. Sherehe kama hii iliandaliwa tena miaka arobaini na mitatu iliyopita baada ya Sugu Senior kuachiliwa huru.
Watu washaanza kufika. Sugu Junior ndiye anatarajiwa kufika wa mwisho baada ya wageni wengine. Zuhura ni mmoja wa wananchi waliofika kushuhudia. Uwanja umegawa pande mbili, kwa viongozi na kwa wananchi. Upande wa viongozi una hema, viti vizuri na soda na maji huku wananchi wakipigwa na miale mikali ya jua.
Muda unasonga, na kufikia saa sita, viongozi waalikwa hawajafika ila wachache tu. Hata viongozi wa majimbo jirani waliolipiwa nauli hawajafika. Watu wameanza kuchoka lakini mfawidhi anawatuliza. Hatimaye Sugu anafika chini ya ulinzi mkali. Anapigwa na butwaa kuona hali ilivyo. Jioni hiyo, mada kuu katika vyombo vya habari ni taarifa ya viongozi kususia sherehe za kuapishwa kwa Sugu Junior.
Ufaafu wa anwani ‘Msiba wa Kujitakia’
Msiba ni tukio linalosababisha huzuni tele na kilio kingi kwa wahusika. Msiba wa kujitakia ni sehemu ya methali inayosema kuwa ‘Msiba wa kujitakia hauna kilio’. Mada hii basi inarejelea matatizo yanayomkumba mtu kutokana na matendo yake mwenyewe.
Machoka anapitia hali ngumu kimaisha. Ametoka kutafuta kibarua lakini hajaambulia chochote, hata cha kutia tumboni. Wakazi wengine wa jimbo hili pia wanapitia hali ngumu kama hiyo. Hali yao ni Msiba wa Kujitakia, kwa kuwa wanfanya uchaguzi bila kuzingatia vigezo vinavyofaa kupata kiongozi anayefaa.
Machoka anakumbuka shairi la Malenga Mteule alilowahi kusoma mahali fulani. Shairi hili linahusu msiba wa kujitakia. Kibwagizo chake ni ‘Msiba wa kujitakiya, kweli hauna kiliyo’. Linaoana na hali ilivyo katika jimbo la Matopeni. Linaongelea visanga vilivyojaa nchini watu wakifilisika. Mtunzi anamwomba Rabana awafungue macho ili waweze kuona.
Kauli ya Zuhura ni ithibati kuwa hali yao ni msiba wa kujitakia. Anamwambia Machoka kuwa wanafaa kumchagua kiongozi wa ukoo wao hata kama hafai kwa kuwa ni mtu wao. Sasa hivi, Zuhura anajutia uamuzi wake huo kutokana na dhiki inayomkumba.
Ugomvi kati ya Zuhura na Machoka ni msiba wa kujitakia. Wanatofautiana kwa kuwa wana misimamo tofauti katika uchaguzi wa viongoiz. Ajabu ni kuwa baada ya uchaguzi, dhiki inawaleta pamoja kwani viongozi wenyewe hawawajibiki kwa vyovyote vile.
Wakazi wa Matopeni wanaruhusu jimbo lao kugeuzwa ngome ya watu fulani wanaowania uongozi. Wanarauka asubuhi na mapema na kustahimili jua la mchana ili kuwapigia kura viongozi, ambao baadaye wanawapuuza na kutojali matatatizo yao. Zuhura anakiri kuwa walikosea kwa kumchagua kiongozi kwa kuwa aliwanunulia vijizawadi vidogo vidogo. Anasema kuwa yanayowakumba ni zao la kumchagua kiongozi kutumia matumbo badala ya akili. Wao ni msiba wa kujitakia.
Fumo Matata anawakumbusha wakazi wa Matopeni kuwa si busara kuwachagua viongozi kwa kuzingatia koo, kwani hali hiyo inaendeleza uongozi mbaya. Hata hivyo, wanampuuza na kumteua Sugu Junior kuwa kiongozi. Wanazidi kutaabika kutokana na mapuuza yao hata baada ya kuonywa.
Zuzu Matata kukosa uongozi wa Matopeni ni msiba wa kujitakia. Anapendekezwa na walowezi kutwaa uongozi lakini anasisitiza kuwa lazima Sugu Senior kwanza aachiliwe kutoka gerezani. Anapoachiliwa, anakuwa maarufu kumliko na kutwaa uongozi. Anakosa fursa nyingine ya kutwaa uongozi huo na kubakia kuwa mpinzani wake hadi kifo chake.
Wananchi wanakubali kukandamizwa. Wanatengewa upande wa kiwanja wanapoadhibiwa na jua huku viongozi wakitengewa upande wenye hema na kuongezewa vinywaji na ulinzi. Wanakubali kukaa siku nzima wakimsubiri kiongozi wao huku wakiumizwa na jua hilo.
Sugu anakosa washirika katika hafla ya kuapishwa, licha ya kuwalipia nauli ya ndege viongozi wa majimbo jirani. Huu ni msiba wa kujitakia, kwani hatilii maanani maslahi ya wananchi. Anataka kuwatumbuiza viongozi kutoka nje kwa fedha za walipa ushuru. Hali hii pia inatokana na ushindi wake anaopata kupitia mlango wa nyuma.
Dhamira ya Mwandishi
Kuwaonya wapiga kura dhidi ya kuwachagua viongozi kwa kutegemea misingi ya kikabila na zawadi wanazowapa na badala yake kutumia vigezo muhimu kama uwajibikaji na kujali maslahi yao.
Anadhamiria kuwatoa matongo wananchi wanaozozana kwa sababu ya misimamo yao tofauti kuhusu viongozi kwani mwisho wa siku ndio wanaobaki katika taabu, na hatimaye dhiki yao itawaleta pamoja tena.
Kuwakanya viongozi wanaotwaa uongozi kupitia mlango wa nyuma na kuendeleza ukoloni mamboleo na udikteta kwamba siku yao ya kulipia maovu hayo itafika.
Kudhihirisha hali halisi inayowakumba Waafrika na binadamu kwa jumla kutokana na maamuzi yao wenyewe.
Anasawiri utofauti uliopo katika jamii nyingi kutokana na toafuti za kiuchumi kati ya watu.
MAUDHUI UTABAKA
Jamii ya jimbo la Matopeni imegawanywa katika makundi mawili makuu kwa kutegemea hali ya kiuchumi. Kuna wenye hadhi na kina yakhe kwa kutegemea hadhi yao katika jamii. Wananchi ambao ndio wapiga kura na watozwa ushuru wako katika kundi la chini linalohangaikia maisha kila uchao.
Maisha kati ya makundi haya mawili tunaambiwa kuwa yametengana kama mbingu na ardhi.
Baada ya ahadi za uongo, viongozi wanatwaa nyadhifa zao na kujiendea kuishi kwa fahari.
Zuhura na Machoka wanalazimika kurejelea uhusiano wao mzuri baada ya uchaguzi. Tunaambiwa kuwa dhiki ndiyo inayorejesha uhusiano wao ambao unavurugwa awali na misimamo yao inayokinzana kuhusiana na viongozi wanaopendelea. Wanagundua kuwa wako katika kundi moja kijamii, kundi la wasakatonge wala viongozi wanaopigania hata hawayajali maslahi yao.
Utabaka pia unadhihirika katika safu ya uongozi. Inavyooonekana, ni kana kwamba kuna wale waliozaliwa kuongoza huku wengine wakiwa wafuasi. Katika jimbo la Matopeni, Sugu Junior na Fumo Matata ndio wanaozozania nafasi ya kuongoza. Nafasi hizi wanaridhi kutoka kwa wazazi wao. Sugu Senior, babake Sugu Junior ndiye alikuwa kiongozi wa matopeni baada ya walowezi kuondoka, hali Zuzu Matata, babake Fumo Matata akiwa mpinzani wake. Yashangaza kuwa ni familia hizo mbili tu zinazozozania uongozi hadi sasa.
Hali ya utabaka pia inaonekana katika mkutano wa kumwapisha Sugu Junior. Kiwanja kimegawanywa mara mbili. Kuna upande uliotengewa wenye ulwa katika jamii kama mawaziri, viongozi wa serikali na viongozi wa majimbo jirani. Upande huu umewekwa hema la kuwazuia jua, kuna vinywaji na walinzi pia. Upande wa pili ni ule wa raia wa kawaida. Huko, jua linawateketeza inavyofaa. Isitoshe, wanalazimika kufika mapema kusubiri kiongozi wao, ambaye anafaa kuwasili mwisho wa wote. Anapofika, yuko na walinzi wanaoimarisha usalama wake, tena anafika saa sita. Usaliti
Jimbo la Matopeni linadhihirisha usaliti wa viongozi waliochaguliwa kwa matumaini ya kuboresha maisha ya wananchi. Wakati wa kupiga kampeni, wanatoa ahadi si haba ambazo wanaahidi kutimiza pindi tu wakiingia mamlakani. Wanaaahidi kuimarisha sekta ya afya, kutengeneza barabara, kuimarisha ukulima, elimu na kuwapa kina mama mikopo ya kuanzisha biashara pamoja na ajira kwa vijana. Hata hivyo, wanasahau ahadi hizi zote wanapoingia mamlakani na kuwatelekeza wananchi waliowachagua.
Zuhura na Machoka wanasaliti demokrasia, jimbo lao na kujisaliti wenyewe wanapochagua viongozi wasiofaa. Zuhura anamwambia Machoka kuwa wanafaa kumchagua mtu wao, awe anafaa au la.
Wanazozana kutokana na misimamo yao inayotofautiana kuhusiana na viongozi wanaotaka. Ajabu ni kuwa viongozi hao hawawafaidi kwa lolote. Zuhura anakiri kwamba walikosea kwa kuwachagua viongozi kwa misingi ya kikabila na pia kwa kuwaziba macho kwa vijizawadi vidogovidogo. Hatimaye wanabaki katika dhiki na kurejesha ujirani wao.
Wahesabu kura pia wanasaliti demokrasia na wapiga kura kwa kuwalimbikiza viongozi wasiotaka. Tunaambiwa kuwa pale Matopeni kupiga kura na kutopiga ni mamoja kwani uamuzi wa mwananchi hauheshimiwi. Tunaambiwa kuwa zoezi la kuhesabu kura ndilo muhimu, na kuwa hata wafu hutoka maziarani wakapiga kura na kurejea huko huko. Ina maana kuwa uamuzi wa wananchi unapuuziliwa mbali na kupatiwa viongozi wasiowafaa.
Viongozi wa majimbo jirani wanamsaliti Sugu Junior kwa kususia sherehe yake ya kuapishwa, licha yake kugharamia nauli zao za ndege. Sugu anawasili saa sita, kwani ndiye anatarajiwa kufika wa mwisho kulingana na itifaki. Anashangaa kuwa ukumbi wa viongozi ukona watu wachache tu, licha ya kuwa amewalipia nauli ya ndege. Nauli ambayo anawalipia kufuta shauku yao kuwa alipata uongozi kupitia mlango wa nyuma. Nauli ya pesa za wananchi, wapiga kura, watozwa ushuru.
Ukabila na Unasaba
Wakati wa kampeni, Zuhura anamwambia Machoka kuwa wanastahili kumchagua mtu wao, awe mzuri au mbaya, awe amesoma au la. Hoja yake ni kuwa wanastahili kuchagua mtu kwa kuwa anatoka kabila lao tu. Mfumo uu unawaletea matatizo mengi kwani huyo mtu wao hajali maslahi yao hata kidogo.
Anatarajia kuwa serikali ya mtu wao itawafaa lakini wapi, wanabakia katika lindi la umaskini bado. Zuhura anakiri makosa yake ya kumchagua kiongozi kwa kuwa ni wa kabila lao. Bado matatizo yanawazidi. Mahitaji yanazidi kuwakaba huku mapato yao yakimegwa na ushuru unaopanda kila uchao.
Katika mahojiano na Radio Salama iliyopo Matopeni, kiongozi wa upinzani Fumo Matata anawakanya wanannchi dhidi ya mfumo wa kupiga kura kwa kuegemea kwenye misingi ya kijinsia. Anawaeleza kuwa mfumo huo umepitwa na wakati na bado wataendelea kutaabika chini ya uongozi wa mtu huyo licha ya kuwa wa jamii yao. Fumo anawaona kama miti ambayo inakubali kuangamizwa na shoka huku ikidhani na mwenzao kwa kuwa mpini wake umetokana nao. Wananchi wanapuuzilia mbali usemi wake na kuendeleza mtindo huo wa uchaguzi, hali ambayo inawaletea matatizo mengi. Wanazidi kutaabika.
Ni wazi kwamba suala la ukabila lilianza pindi tu baada ya kuondoka kwa walowezi wala si jambo geni. Tunaambiwa kuwa baada ya walowezi kuondoka, Zuzu Matata anaazimia kuchukua uongozi na kupendekezwa na walowezi. Hata hivyo, anasisitiza kwamba Mzee Sugu Junior aachiliwa kutoka jela alikofungwa. Anapoachiliwa, anapata umaarufu kumliko. Tunaambiwa kuwa Sugu alitwaa uongozi kwa shuruti za wazee wa kabila lake.
Hali ya unasaba pia inadhihirika katika uongozi wa jimbo la Matopeni. Mzee Sugu Senior anatwaa uongozi huku Zuzu Matata akiwa mpinzani wake. Baada yao kufariki, wanao wanachukua nafasi zao katika taifa. Sugu Junior, mwanawe Sugu Senior, anatwaa uongozi huku Fumo Matata, mwanawe Zuzu Matata akiwa mpinzani wake wa karibu. Inastaajabisha kuwa ni familia mbili tu ambazo zinazozania uongozi wa Matopeni, ni kana kwamba ndizo zilizaliwa kuongoza na hakuna familia nyingine inayoweza kuchukua uongozi huo.
UKOLONI-Mwongozo Wa Mapambazuko ya Machweo
Kuna sura mbili za ukoloni katika hadithi; Ukoloni Mkongwe na Ukoloni Mamboleo. Tunasimuliwa kuwa wakati fulani huko nyuma, jimbo la Matopeni lilikuwa limetawaliwa na walowezi, lakini hatimaye wakatimuliwa. Walikuwa wamemweka kizuizini kiongozi Mzee Sugu Senior lakini Zuzu Matata akampigania hadi kuachiliwa, kisha akachukua uongozi baada ya kuachiliwa kutoka seli. Hatimaye jimbo la Matopeni likawa huru.
Hata hivyo, bado ukoloni unaendelezwa na waliotwaa uongozi kutoka kwa walowezi. Viongozi wa Matopeni hawajali maslahi ya wanyonge wanaowachagua. Wanapania kujinufaisha tu. Wanajitenga nao na kujiboreshea maisha huku wapiga kura wakizidi kutaabika. Wanawatoza ushuru ambao wanatumia vibaya kama vile kulipia nauli ya viongozi majirani kuja katika sherehe za kuapishwa kwa Sugu Junior.
Ukoloni Mamboleo pia unaonekana kupitia shughuli ya uchaguzi wa viongozi. Wananchi wanaruhusiwa kupiga kura lakini kura zao hizo hazitiliwi maanani, licha yao kuvumilia jua kali kuteua chaguo lao.
Inasikitisha kuwa baada ya hayo yote, bado kura zao hazitiliwi maanani bali wanalimbikiziwa viongozi wasiowataka. Shughuli ya kupiga kura haitiliwi maanani bali mchakato unaofuata wa kuhesabu kura hukumbwa na tafrani na hatimaye viongozi wasioshinda kuteuliwa, badala ya uteuzi wa wapiga kura kuheshimiwa.
Hali sawa pia inadhihirika katika sherehe za kumwapisha kiongozi Sugu Junior kiwanjani Mamboleo. Viongozi wanastahiwa na kupatiwa hadhi ya juu, kinyume na usawa uliopiganiwa wakati wa kuwafukuza wakoloni. Viongozi wamewekewa hema la kuwasitiri jua na pia kupatiwa vinywaji pamoja na ulinzi wa kipekee, kinyume na wananchi wanaotelekezwa juani. Isitoshe, Sugu Junior anawasili baadaye baada ya wananchi kumngoja kwa kitambo huku wakiunguzwa na jua.
MIGOGORO
Kuna hali ya mgogoro kati ya viongozi na raia kutokana na hali mbaya ya maisha inayowakumba wananchi. Tunaambiwa kuwa mzigo wa maisha ambao Wanamatopeni walikuwa wamebebeshwa walikuwa tayari kuutua. Wanawachagua viongozi ambao wanawatelekeza na kutojali maslahi yao. Wako tayari kupigania haki zao.
Zuhura na Machoka pia wanajipata katika mgogoro. Zuhura anapendekeza kuwa wanafaa kumchagua kiongozi kwa kuwa anatoka katika kabila lao, lakini Machoka ana msimamo wake. Mgogoro huu unaisha baada ya uchaguzi pale viongozi wao wanapowatelekeza na dhiki yao kuwaleta pamoja.
Kuna mgogoro kati ya Sugu Junior na Fumo Matata, wawaniaji wakuu wa uongozi katika jimbo la Matopeni. Fumo amekuwa mpinzani wa Sugu, na sasa anawania uongozi kwa mara ya tatu mfulululizo. Serikali inasifia maendeleo iliyoleta lakini upinzani unaona hizo kuwa porojo tupu.
Mgogoro kati ya vinara hawa wawili tunagundua kuwa ulianza kwa wazazi wao, waanzilishi wa jimbo hili. Zuzu Matata, babake Fumo Matata alikuwa mpinzani sugu wa Mzee Sugu Senior, babake Sugu Junior, alipotwaa uongozi baada ya kuondoka kwa walowezi.
Umaskini
Hali ya umaskini inadhihirika katika makazi ya Machoka, akiwa tu kama mfano wa umma mkubwa wa wakazi wa Matopeni. Ametoka katika shughuli za kutafuta kibarua lakini hajafanikiwa. Tumbo linamwuma kwa njaa kwani hajala tangu asubuhi. Inasemekana kuwa taswira ya chumba chake ingeweza kumliza kipofu.
Zuhura ni mfano mwingine wa hali hii. Yeye pia anahisi ugumu wa maisha baada ya viongozi kutotimiza ahadi walizotoa wakati wakampeni. Ushuru nao uko juu na unawakandamiza. Dhiki inarejesha uhusiani mzuri kati yake na Machoka uliovurugwa na misimamo yao tofauti wakati wa uchaguzi.
Maudhui mengine ni kama vile Ufisadi, Kutowajibika, Udhalimu na Uongozi Mbaya.
Wahusika: Sifa na Umuhimu Machoka
Ni mwenye bidii. Anarauka asubuhi na mapema kwenda kusaka kibarua ili kukidhi mahitaji yake. Hakati tamaa hadi jioni anapokosa kabisa.
Ni mkakamavu. Anaposhikilia lake, habanduki. Ana msimamo wake katika uchaguzi wala kauli ya Zuhura haibadilishi msimamo wake. Anahiari kukosana naye badala ya kufuata ushawishi wake.
Ni mzalendo. Siku ya kupiga kura, anaungana na Wanamatopeni wengine kwenda kupiga kura kwa nia ya kumteua kiongozi wao.
Ni mwenye kumbumkumbu. Anapokinai hali yake, anakumbuka shairi alilowahi kusoma kuhusiana na msiba wa kujitakia lililoandikwa na mshairi mwenye lakabu ya Malenga Mteule. Umuhimu wa Machoka
Ni kiwakilishi cha mateso wanayopitia raia chini ya utawala mbaya
Ni kielelezo cha bidii na kujituma katika shughuli licha ya matatizo ya maisha. Anadhihirisha mgawanyiko uliopokatika jamii kwa misingi ya kiuchumi na mamlaka. Zuhura
Ni mzalendo. Siku ya kupiga kura, anrauka bukrata na wenzake kwenda kupanga foleni na kusubiri hadi zamu yao kupiga kura ili kumteua kiongozi wao.
Ni mshawishi. Anamsisitizia Machoka kuwa wanafaa kumchagua kiongozi kutoka kabila lao. Anapokataa wanazozana.
Ni mkabila. Ananuia kuteua kiongozi kutoka kabila lake. Hajali iwapo kiongozi huyo ni mzuri au mbaya, amesoma au la.
Ni mvumilivu. Ni mmoja wa wale wanaosubiri ujio wa Sugu Junior katika sherehe za kuapishwa kwake. Anaunguzwa na jua na kusubiri, hata hina mikononi na wanja machoni unaanza kuyeyuka lakini anangoja hadi kiongozi anapofika.
Ni mkakamavu. Anapofanya uamuzi hatetereki. Anakata kauli kumteua kiongozi kutoka katika kabila lake. Anangoja hadi kiongozi anapofika katika sherehe za kuapishwa kwa Sugu Junior.
Umuhimu wa Zuhura.
Anadhihirisha jinsi raia wanavyochangia katika matatizo yanayowakumba kwa kuwachagua wasiofaa. Ni kiwakilishi cha ukabila na mchano wake katika kuiangusha jamii.
Kupitia kwake, mgawanyiko wa kijamii kwa misingi ya kiuchumi unadhihirika. Ni kiwakilishi cha matatizo wanayopitia raia wa kawaida katika nchi.
Sugu Junior
Ni fisadi. Anawaacha wananchi waliompa wadhifa kutaabika wala hajali maslahi yao. Anatwaa uongozi kwa njia za kifisadi kwani siye chaguo la wananchi
Ni mbadhirifu. Anatumia visivyo hela za jimbo la Matopeni. Anawalipia nauli viongozi wa majimbo jirani kuja katika sherehe za kuapishwa kwake, sherehe ambazo hata hawaji.
Ni mwenye tamaa. Ana tamaa ya uongozi. Anatumia kila njia kuhakikisha kuwa ametwaa uongozi japo siye chaguo la wananchi.
Ni mnafiki. Wakati wa kampeni, anajinasibisha na watu na hata kuwa karibu nao ili kupata kura zao. Anapopata mamlaka, anajitenga nao kama mbingu na ardhi.
Umuhimu wa Sugu
Ni kiwakilishi cha viongozi wasiojali maslahi ya umma uliowachagua.
Kupitia kwake, hali ya mvutano katika uongozi inadhihirika na jinsi hali hiyo inavyoathiri maendeleo Ni kiwakilishi cha unafiki wa viongozi wengi katika jamii Ni kiwakilishi cha ukoloni mamboleo katika jamii ya sasa.
Fumo Matata
Ni mkakamavu. Anapoamua kuwania uongozi, harudi nyuma licha ya kufeli. Anafeli mara mbili lakini bado yuko debeni kwa mara ya tatu.
Ni mwenye bidii. Anazunguka kote Matopeni akiimarisha kampeni zake na kutwaa wafuasi wengi.
Ni mwenye maono. Watu wanapendezwa sana na mipango yake aliyoweka ya kuwaboreshea maisha na wako tayari kumchagua kwa ajili hiyo.
Umahimu wa Fumo
Ni kiwakilishi cha viongozi wanaojaribu kwa kila hali kupigania maslahi ya wananchi wanaoteseka. Kupitia kwake, hali ya ukoloni mamboleo inadhihirika ilivyokita mizizi katika jamii
Anadhihirisha mizozo iliyopo ya uongozi na athari yake katika jamii.
Ni kiwakilishi cha imani na tumaini la usawa wa kijamii katika siku zijazo.
Mbinu za Uandishi. Tashbihi
Maisha kati ya makundi haya mawili, yaani mpiga kura na mpigiwa kura, yametengana kama mbingu na ardhi.
Anasimama pale kama kigingi
Zuhura na Machoka walikuwa kama fahali wawili-hawakai katika zizi moja.
Maisha ya Wanamatopeni yalikuwa kama mchezo wa karata, hawajui leo wala kesho.
Wanamatopeni walipotathmini hali zao, walijifananisha na panya walionaswa kwenye mtego wa uhitaji. Fumo aliona hali ya Matopeni kama kisa cha msitu na shoka.
Wakishapata walichokitaka, walijitenga na umma kama wagonjwa wa ukoma. Semi
zimegonga mwamba- zimekosa kufanikiwa kukodoa macho- kufungua macho yote
ndoto iliyozikwa katika kaburi la sahau- iliyosahaulika vinywa wazi- wameachama, kwa
mshangao
kula halafa- kuapa/kuapishwa wakipiga doria- wakiimarisha ulinzi Methali
Punda akichoka, mzigo huutua. Lisilobudi hubidi
Wajinga ndio waliwao
Mzigo wa mwenzio ni kanda la usufi Ukistaajabu ya Musa, hujayaona ya Firauni Subira huvuta heri.
Majazi
Machoka-mhusika huyu amechoshwa na maisha ya umaskini. Ametoka kutafuta kibarua mchana kutwa huku amechoka. Yuko tayari kutua mzigo aliotwishwa, ambao umemchosha.
Zuhura- ni sayari ya pili kutoka kwenye jua. Anajiona kuwa karibu na jua(uongozi), eti kwa sababu kiongozi anatoka kabila lake. Yuko kwenye mstari wa mbele kupiga kura na pia katika sherehe za kuapishwa kwa Sugu Junior.
Matopeni-ni jimbo la watu wanaong’ang’ania maisha yao. Kumejaa tope la umaskini, ujinga, unyanyaswaji na ukabila, miongoni mwa mengine.
Sugu Senior. Sugu ina maana ya ‘siyoweza kubadilika kwa urahisi’, au ‘siyosikia dawa’. Mzee Sugu anatwaa uongozi na kuushikilia bila kutetereshwa na upinzani wa Zuzu Matata. Senior ni kuwa ndiye mkubwa kati ya Sugu wawili kwenye hadithi.
Sugu Junior. Mwanawe Sugu senior anayeendeleza ubabe wa babake dhidi ya mpinzani wake, Fumo Matata.
Zuzu Matata. Zuzu ina maana ya mjinga. Anapigania Sugu Senior kutolewa seli, na anapotolewa, anamnyang’ama uongozi. Hili linamletea matatizo mengi(Matata) hadi anapokufa bila kuonja ladha ya uongozi.
Fumo Matata. Ni mwanawe Zuzu Matata. Fumo ni aina ya mkuki unaotiwa kwenye upande mmoja wa mpini, au kiongozi wa kijadi. Ni mkuki wa Matopeni wa kuboresha maisha lakini hapati fursa hiyo. Pia ni kiongozi kwa kuwa anachaguliwa na raia lakini anapokwa nafasi yake.
Mamboleo. Ni uwanja anaofaa kuapishwa Sugu Junior. Hii ni shughuli ya kileo. Pia, viongozi wanafanya mambo kileo wanaposusia sherehe hizo. Wamechoshwa na wizi wa kura.
Kinaya
Wakati wa kampeni, serikali inajigamba ilivyoleta maendeleo. Ukweli ni kuwa haijaleta maendeleo yoyote.
Zuhura anamwambia Machoka kuwa wanafaa kumchagua mtu wao, awe mzuri au mbaya. Ajabu ni kuwa wao ndio wanateseka chini ya uongozi huo.
Zuzu Matata anampigania Mzee Sugu Senior kutolewa seli. Kinaya ni kuwa anapotoka, anapata umaarufu kumshinda na kutwaa uongozi. Wanaishia kuwa wapinzani badala ya kushirikiana.
Tunaambiwa kuwa pale Matopeni kupiga kura na kutopiga ni mamoja kwani uamuzi wa mpiga kura hauheshimiwi. Sasa kuna haja gani ya zoezi hilo basi? Shughuli muhimu ya kidemokrasia inageuzwa kuwa mzaha.
Uwanjani Mamboleo, sehemu ya viongozi imeimarishwa kwa hema, viti, vinywaji na ulinzi.
Wananchi wanatelekezwa kwenye jua, hali ndio watoa ushuru.
Viongozi wa majimbo jirani wanasusia sherehe za kuapishwa kwa Sugu Junior hata baada yake kugharamia nauli yao ya ndege.
Kisengerenyuma/Mbinu Rejeshi
Machoka anapokinai matatizo ya maisha, anakumbuka shairi alilowahi kusoma la Malenga Mteule.
Machoka pia anakumbuka mambo yalivyokuwa wakati wa kampeni. Anakumbuka ahadi ambazo walipatiwa, jinsi serikali ilivyojisifia kuleta maendeleo huku upinzani ukikejeli kauli hiyo.
Anakumbuka pia kauli ya jirani yake Zuhura kuwa wanafaa kumchagua mtu wao, awe mzuri au mbaya, amesoma au la. Anakumbuka hali ya suitafahamu kati yake na Zuhura huyo kutokana na misimamo yao hiyo, hali iliyoyeyushwa na dhiki baada ya uchaguzi.
Tunarejeshwa kwa historia ya Matopeni baada ya kutwaa uhuru, huku Mzee Sugui Senior akiingia mamlakani baada ya kupiganiwa na Zuzu Matata kutolewa seli, upinzani wao katika safu ya uongozi hadi kufariki kwa Zuzu Matata bila kuonja ladha ya uongozi.
TAKRIRI
Anawaza juu ya maisha yake. Maisha ya wasakatonge. Maisha ya wanaojiita ‘pangu pakavu’. Maisha ya wapiga kura. Maisha ambayo ni tofauti sana na maisha ya waliowapigia kura. Maisha kati ya makundi haya mawili…
“Wetu ni wetu, hata akiwa mbaya ni wetu… Awe amesoma au hajasoma, angali wetu.” Leo hii amebaki kujuta. Kujuta ghaya ya kujuta!
Tayari alikuwa amekwishafanya kosa. Kosa ambalo lilikuwa la kujitakia.
Hivyo ndivyo ari yake Zuzu Matata ya kuiongoza Matopeni ilivyogeuka kuwa ndoto. Ndoto inayosemekana ilizua uhasama mkubwa kati ya viongozi hawa wawili. Ndoto iliyomfanya Zuzu Matata kuwa mpinzani… Ndoto anayozidi kuiota akiwa mle kaburini. Ndoto iliyozikwa katika kaburi la sahau.
Ila kesho…kesho…kesho yote haya yatakuwa marehemu…
Zuhura amechukua nafasi yake kwenye sehemu ya pili…, sehemu ambapo jua kali lilipenyeza miale…,
sehemu ya wapiga kura… “Subira…subira…subira…ndugu zangu.” Tashihisi
Machoka anabaki kukodoa macho huku maonevu yakiihukumu nafsi yake. Kongole kwa ‘ushindi’ wako, ingawa ushindi huo huenda usione jua!
Ukumbini, viti vinamkodolea macho.
Hadithi ndani ya Hadithi
Tunasimuliwa kisa cha msitu na shoka. Miti katika msitu iliangamizwa na makali ya shoka huku ikifurahia eti kwa kuwa mpini wa shoka ulitokana na mmoja wao. Ilidhani shoka ni mwenzao. Kisa hiki kinafananishwa na Wanamatopeni wanaomchagua kiongozi kwa misingi ya kikabila ila anawadhulumu wakidhani ni mmoja wao.
CHUKU
Taswira ya chumba chake ingeweza kumliza kipofu.
Hata hina aliyokuwa amejiremba Zuhura mikononi na wanja aliokuwa amejipaka imekwishaanza kudondoka kwa makali ya jua.
Ulinzi mkali ambao ungemzuia hata nzi kupita karibu naye! Kejeli
Mzigo wa maisha haukuwatisha wala kuwakosesha usingizi viongozi wao Ndoto anayozidi kuiota akiwa mle kaburini!
Pale Matopeni, siku hizi hata wafu hupiga kura na kurejea maziarani!
Sherehe hii bila shaka imeigharimu serikali mabilioni ya pesa. Pesa za walipaushuru, kina yakhe kama Machoka na Zuhura.
Zuhura amechukua nafasi yake kwenye sehemu ya pili, palipoandaliwa kwa ajili ya watu kama yeye, sehemu ambapo jua kali lilipenyeza miale yake ya ghadhabu, sehemu ya wapiga kura, watozwa ushuru! Koja
Tunaahidi kutengeneza barabara, kuimarisha sekta ya afya, kuinua kina mama wetu kwa kuwapa mikopo ya kuanzisha biashara…
…kaka, ndoto haifi ila vizingiti haviishi daima; kulimbikiziwa viongozi, udikteta, ukoloni mamboleo…
Mizani ya ubora wa kiongozi haitakuwa kabila lako, ukoo wako, familia yako, nani unayemjua, una hela ngapi…
Mbinu nyingine ni pamoja na Ushairi, Tabaini, Mdokezo, Maswali Balagha, Nidaa, Kuchanganya Ndimi, Tanakali, Lakabu na Ujumbe wa Simu.
Mapambazuko ya Machweo- Clara Momanyi Mtiririko.
Mzee Makucha na Mzee Makutwa ni marafiki, ambao wamestaafu na umri wao umesonga. Hata hivyo, urafiki wao uliokolea awali sasa umepungua, umebaki tu ule wa kujuliana hali. Mzee Makutwa anaonekana akizurura mtaani na gari lake baada ya kustaafu, wala hakuna ajuaye shughuli zake, hata Mzee Makucha. Anaonekana tu kila mara akiwabeba vijana garini, wala haijulikani anawapeleka wapi. Mkewe Makucha, Bi Macheo anamsaili mumewe kuhusiana na hili lakini hapati taarifa yoyote. Makutwa anajinaki kuwa hawezi kuishi maisha ya kutaabika hata kama amestaafu. Bi. Macheo anamshauri mumewe akomeshe urafiki na Mzee Makutwa, lakini mumewe anamweleza kuwa urafiki uliobaki kati yao ni wa salamu tu.
Mzee Makucha anauza vitafunio kwenye makutano ya barabara baada ya kustaafu kutoka kazi yake alipopigwa kalamu. Anafanya kazi na shirika la reli lakini linasambaratika baada yake kuachishwa kazi, hivyo juhudi zake kwenda mahakamani ni bure. Akiwa kazini kwake(kuuza vitafunio), anashangazwa na kazi anayofanya Makutwa, ambaye anatangamana na vijana kila uchao wala hana hata muda wa kuwasabahi wazee wenzake.
Mzee Makutwa anafika katika kazi ya Mzee Makucha na kutapakaza vumbi kwenye vitafunio vyake kwa gari lake akilipiga breki. Anamkejeli Makucha, akimwambia kuwa anafaa kujipumzisha nyumbani na kazi hiyo kuachia vijana. Lakini Makucha anamsisitizia kuwa yuko sawa nayo, kuliko yeye anayezurura mitaani na vijana. Anamdhihaki kuhusu bintiye aliyetoroshwa na Mhindi, huku akimkumbusha afurahie maisha licha ya matatizo. Mashaka ya Makucha kuhusu kazi afanyayo Makutwa yanazidi.
Vijana wawili, Dai na Sai wananunua kashata kwa Makucha na kuelezana kuhusu taabu za maisha baada ya kufuzu na kukosa kazi. Wanaamua kujaribu bahati yao na gari la probox linalozunguka likikusanya vijana. Makucha anajua bila shaka ni gari la Makutwa. Gari linapofika wanalipungia mkono na kuingia.
Linaendeshwa na kijana sasa hivi, sio Makutwa.
Makucha anamwita mkewe kuchukua vitu vyake na kuchukua teksi kulifuata gari lile. Wanasafiri hadi wanapoingia kwenye mgodi wa kisiri uliofichwa katika mazingira makavu. Anaingia kwenye mgodi na kushuhudia jinsi vijana wanavyodhalilishwa humo kwa kazi ya kutafuta madini. Anarudi tena na kuwadanganya walinzi kuwa anamtaka Mzee Makutwa, ambaye huku anaitwa Mzee Mamboleo.
Anawaaga akidai atamfuatilia nyumbani.
Anarudi mjini Kazakamba na kuripoti polisi, ambao wanaandamana naye hadi kwenye lile pango. Wanamkuta Mzee Makutwa akikagua mgodi. Anatokomea pangoni na kupotelea humo, hadi polisi wanapomrushia vitoza machozi. Anatoka akikohoa na kufungwa. Anamlaumu Mzee Makucha kwa kumwendea kinyume, lakini naye anamwambia haki ndio muhimu. Hatimaye anatupwa korokoroni kwa kosa la jinai.
Mzee Makucha anapokea zawadi ya hundi ya pesa kutoka kwa tajiri mmoja anayeendeleza miradi ya maendeleo kwa vijana. Anayaona haya kama mapambazuko mapya, licha ya maisha yake kuwa katika machweo.
Ufaafu wa anwani ‘Mapambazuko ya Machweo’.
Mapambazuko ni wakati wa asubuhi inapoingia na jua kuchomoza. Machweo nao ni wakati wa jua kutua na giza kuingia. Mada hii inaweza kufasiriwa kuwili; mapambazuko yanayotokea wakati wa machweo, au mapumbazuko yaliyo katika machweo. Dhana hizi, mapambazuko na machweo pia zimetumiwa kwa maana nyingine. Mapambazuko yanawakilisha wakati wa ujana, huku machweo yakiwakilisha uzee. Pia, mapambazuko yanaashiria mwangaza(fanaka) huku machweo yakiashiria giza(taabu/mashaka).
Makutwa anawashangaza wengi kwa kuwa anashinda na vijana kila wakati licha ya kuwa ni mzee. Hashirikiani na wazee wenzake hata kidogo. Anaonekana kama ujana wake umeingia akiwa mzee, yaani mapambazuko yake yanamjia akiwa katika machweo.
Mzee Makucha anafanya biashara ya kuuza vitafunio. Japo Mzee Makutwa anamkejeli, yeye anaiona kuwa ndio tumaini lake baada ya kufutwa kazi kwenye shirika la reli. Machweo yanaingia kwa kuachishwa kazi, na anaiona biashara hii kuwa mapambazuko yake.
Binti yake Makucha, Riziki, anaolewa na kigogo Mhindi baada ya kushindwa kuvumilia dhiki.
Kutokana na machweo ya umaskini, anaonelea ndoa hiyo kama mapambazuko kwake.
Mzee Makucha anamweleza Mzee Makutwa kuwa siku moja, jua la macheo(Mapambazuko) litambishia mlango japo anaelekea machweo. Yaani, ipo siku atafanikiwa licha ya uzee wake.
Sai na Dai wanaeleza taabu ya maisha yao. Ni miongoni mwa vijana waliohitimu kutoka chuo kikuu na kukosa kazi. Wanazurura tu mitaani. Wako karibu kukata tamaa. Machweo yameanza kuwaingilia katika maisha hali bado wako wakati wa mapambazuko. Wanaona shughuli za probox ya Makutwa kama nafuu ya pekee, yaani mapambazuko ya kuwatoa katika machweo waliyomo.
Mzee Makucha anapofuata gari la Makutwa kwa teksi, linawaongoza hadi kwenye mgodi mkubwa, ambapo vijana na watoto wadogo wanafanya kazi ya kusaka vito vya thamani. Wanapata taabu nyingi, na wengi wao wanakosa hata fursa ya masomo. Machweo yameshaingia katika maisha yao hali wako katika mapambazuko.
Mzee Makutwa amewatesa vijana wengi kwa kuwaingiza katika machweo ya kumfanyia kazi ya kinyama ya kusaka vito. Hawana imani ya maisha bora. Kukamatwa kwake na polisi ni mapambazuko ya machweo, kwani uovu wake unafikia kikomo.
Mzee Makucha anapata zawadi ya hundi kutoka kwa tajiri mmoja anayeendeleza miradi ya kuwainua vijana kimaendeleo. Amekuwa akiishi kwa taabu kwa kuuza vitafunio kando ya barabara. Haya ni mapambazuko(mafanikio) ambayo yanamwangukia katika machweo ya maisha yake(uzee na taabu).